27.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga yashikwa Mbeya, Simba mpaka raha

YangaSimbaNA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM, MBEYA

WAKATI timu ya Yanga ikibanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya maafande wa Prisons katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, Wekundu wa Msimbazi Simba wameendelea kung’ara na kujiimarisha katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya timu ya Mgambo Shooting mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 40 ikiendelea kuwa kileleni mwa msimamo huo huku timu ya Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na ponti 39 sawa na timu ya Azam, wakitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, Simba ikiwa mbele kwa mabao ya kufunga 32, Azam 30 lakini pia wana lambalamba hao wana viporo vya mechi mbili mkononi.

Katika mchezo wa Dar es Salaam, mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na Hamis Kiiza (dk 5 na 83), Mwinyi Kazimoto (dk 28), Ibrahim Ajib (dk 43) na Dan Lyanga (dk 78), wakati la Mgambo lilifungwa Full Maganga (dk 89).

Kiiza alifunga bao hilo la mapema baada kupokea pasi kutoka kwa Ajib, lakini dakika nane baadaye Kiiza alitaka kuwatoa roho mshabiki wa Simba baada ya kukosa penalti akipiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa wa Mgambo, Mudathir Hamis. Simba walipata penalti hiyo baada ya beki wa Mgambo aliyekua katika harakati za kuokoa kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Kazimoto aliwainua mashabiki wa Simba baada ya kuandika bao la pili dakika ya 28, alipopiga shuti akiwa ndani ya 18, mpira ulimfikia mfungaji baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Mgambo ambapo Simba waligongeana vizuri pasi na kumfikia mfungaji.

Dakika ya 43, Simba waliongeza bao la tatu kupitia kwa Ajib, aliyempiga kanzu kipa na kujaza mpira wavuni akiwa amepewa pasi safi na Jonas Mkude kabla ya kumkuta kipa.

Simba iliendelea kunoga kwa kuongeza mshambulizi ambapo dakika ya 78, Lyanga aliyeingia  kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ajib aliongeza bao la nne akipiga mpira uliojaa wavuni.

Kiiza alihitimisha karamu ya mabao dakika ya 83 akiunganisha vema krosi ya beki kisiki, Hassan Kessy.

Hata hivyo, Mgambo iliweza kujitutumua na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 89 lililofungwa na  mshambuliaji wake, Full Maganga.

Mchezo wa Yanga na Prisons ulianza kwa kasi timu zote zikionekana kutaka bao la mapema, huku Yanga wakicheza mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Yanga ilifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 35 lililofungwa na Amissi Tambwe, ambapo dakika nne baadaye Prisons walisawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji wake, Jeremiah Juma, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mohamed Mkopi.

Bao hilo kwa Prisons liliongeza ari na kujiamini, hali iliyopelekea kupata bao la pili dakika ya 60 kupitia kwa Mohamed Mkopi, alieunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Seif Kijiko, baada ya Benjamin Asukile kufanyiwa madhambi na Tambwe.

Hali ilianza kuonekana kuwa mbaya kwa Yanga baada ya Prisons kuonekana kuwa bora zaidi lakini ghafla timu hiyo ilianzia kujitutumua dakika ya 70 hadi 80 na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 86 kupitia penalti iliyopigwa na Simon Msuva kufuatia Meshack Seleman kuunawa mpira uliopigwa na Haruna Niyonzima, hivyo mwamuzi Zebron Frontina kutoka Dodoma kuamuru penalti hiyo iliyopelekea matokeo ya sare ya 2-2 dakika 90 zilipomalizika.

Kwenye michezo mingine timu ya Mtibwa ilijikuta ikilazimishwa sare ya 2-2 nyumbani kwao Manungu Turiani na timu ya Toto Africans, African Sports waliutumia wenyeji wao vizuri kwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC, huku Wanalizombe Majimaji ya Songea wakikubali kichapo cha bao 2-1 nyumbani kwao kutoka kwa Kagera Sugar.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles