25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YAPUNGUZWA SPIDI

Na THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM

YANGA  imeshindwa kuondoka na pointi tatu, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo  uliochezeshwa na mwamuzi, Elly Sasii wa Dar es Salaam, bao la Yanga lilifungwa na Mrisho Ngassa, huku Abdul Hillary akiifungia KMC.

Matokeo  hayo, yanaonekana kupunguza kasi ya ushindi kwa Yanga iliyokuwa imeshinda michezo mitatu mfululizo.

Kabla ya mchezo wa jana, Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0  dhidi ya Ndanda uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, kisha ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania, Uwanja wa Uhuru.

Mchezo uliopata Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-1  dhidi ya Alliance, uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

 Kwa matokeo ya jana yameifanya Yanga  kufikisha pointi 17, baada ya kucheza michezo nane, ikishinda mitano, sare mbili na kufungwa mmoja ikishika nafasi ya nane.

Kwa upande wa KMC  inashika nafasi ya 17  kutokana na pointi tisa,  baada ya kucheza michezo 11 ikishinda michezo miwili, sare tatu na kupoteza sita.

Katika mchezo wa jana, Yanga  walikuwa wa kwanza kufika langoni kwa KMC dakika ya saba,  baada ya Patrick Sibomana kupiga shuti, lakini liliokolewa na beki wa KMC Abdlaah Mfuko na dakika tatu baadaye alipiga shuti kali na kutoka nje.

KMC walifanya shambulizi nzuri dakika ya 15, lakini  Mohamed Samatta alishindwa kufunga baada ya kupaisha  shuti lake.

Mshambuliaji wa Yanga, David Molinga, alishindwa kumalizia pasi ya mwisho ya kiungo wa timu hiyo, Papy Tshishimbi  dakika ya 25,  ambaye  alijikuta akiokoa badala ya kufunga.

Molinga alipoteza nafasi nyingine ya kufunga dakika ya 36,  baada ya kumpiga chenga beki wa timu ya  KMC, Kelvin Kijiri na shuti lake kwenda pembeni.

Yanga ilikosa bao dakika ya  38  baada ya kutokea piga nikupige langoni kwa  KMC na Sibomana kupiga shuti lililogonga mwamba na kurudi uwanjani na kumkuta Sadney ambaye naye  aliachia shuti  na kupanguliwa na kipa Jonathan Nahimana na kuwa kona tasa.

KMC walifanya shambulizi nzuri dakika ya 43  na Hassan Kabunda  kufanikiwa kupiga shuti ndani ya eneo la 18 na mpira kutua  mikononi mwa Nahimana.

Dakika mbili baadaye Deus Kaseke wa Yanga  alipiga shuti nje ya eneo la  18,  lakini  kipa wa KMC Nahimana alidaka,

Mwamuzi Sasii alimwonesha kadi ya njano Tshishimbi dakika ya 50 kutokana na kumchezea faulo Samatta aliyeshindwa kuendelea na mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na Abdul Hillary.

Kabunda wa KMC walishindwa kuipatia timu yake bao la kuongoza dakika ya 53 kutokana na kupaisha shuti lake.

Winga wa Yanga, Mrisho Ngassa aliyeingia dakika ya kuchukua nafasi ya Sadney Urikhob dakika ya 46, alifanya kazi nzuri dakika ya 56, lakini Sibomana alishindwa kumalizia baada ya kupiga shuti hafifu na kuokolewa na mabeki wa KMC.

Yanga walipata bao dakika ya 73 kupitia kwa Ngassa baada ya kuwatoka mabeki wa KMC  na kupiga shuti kali lililokwenda moja kwa  moja nyavuni.

Kabunda almanusura alipatie timu yake bao dakika ya 83, baada ya kupiga mpira wa adhabu, hata hivyo uliokolewa na kipa wa Yanga, Farouk Shikalo.

Makosa yaliyofanywa na beki wa Yanga,  Kelvin Yondan kwa kumchezea faulo Kabunda ndani ya eneo la hatari dakika ya 90 na kuiwezesha  KMC kupata penalti iliyofungwa na Hillary.

 Yanga; Farouk Shikalo, Juma Abdul, Jafar Mohammed, Lamine Moro,  Kelvin Yondan,  Ally Mtoni/Mapindizi Balama(dk.71),  Deus Kaseke,  Papy Tshishimbi, David Molinga, Sadney Urikhob/Mrisho Ngassa (dk. 46) na  Patrick  Sibomana

KMC; Jonathan Nahimana, Kelvin Kijiri, Ally, Ramadhani,  Ismail Gambo, Abdallah Mfuko, Kenny Ally, Rayman Mgungila,  Ramadhani Kapera,  Hassan Kabunda,  Serge Noguez  na Mohamed Samatta/Abdul Hillary (dk.50)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles