33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YANUSA TENA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO

Na ABDUL MKEYENGE-DAR ES SALAAM


VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wameanza vyema kwenye mchezo wao wa kwanza wa Shirikisho kwa kuwafunga MC Alger na kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Katika michuano hiyo mwaka jana Yanga iliweza kutinga hatua ya makundi, baada ya kuiondosha  Sagrada Esperanca kwa jumla ya mabao 2-1, ambapo nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam walishinda 2-0 na kuambulia kichapi cha bao 1-0 ugenini.

Yanga imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0, ambalo hivi sasa linawahitaji waende ugenini wakihitaji sare, ushindi wa aina yoyote ili waweze kusonga mbele na wakutane na utajiri mkubwa wa fedha ambao timu hupata ikishatinga hatua ya makundi.

Ni kazi ya wachezaji wa Yanga pamoja na viongozi wao kwenda Algeria kukutana na dakika 90 nyingine za machozi, jasho na damu kwa wakati mmoja ili waweze kutinga hatua hiyo na kuwa sehemu ya historia ya klabu itakayokuja kukumbukwa vizazi na vizazi.

Yanga ina historia mbaya dhidi ya timu za Afrika Kaskazini, lakini ushindi wao wa hapa nyumbani ni faraja kubwa kama wakienda kwenye mchezo wa marudiano wakiwa na mipango ambayo wakati mwingine hukosekana na kujikuta wakirejea nyumbani vichwa chini.

Spotikiki iliufuatilia mchezo huo wa nyumbani kwa dakika zote 90, zilizochezeshwa na mwamuzi Louis Hazikumana wa Rwanda na kubaini Yanga inahitaji baadhi ya marekebisho kwenye mchezo wa marudiano ambao utachezwa Algeria.

Timu kucheza kwa presha

Yanga ilicheza mbele ya mashabiki wake, lakini ilikuwa na presha kubwa iliyoanza kwa mashabiki wenyewe wa kwenda mpaka kwenye miguu ya wachezaji wao ambao hawakuwa na utulivu uwanjani.

Wachezaji wa Yanga walionekana kutaka bao la mapema ili kuwafanya MC Alger wakae chini kujilinda, hali hii iliwafanya wachezaji wacheze bila kuwa makini na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga ambazo kama ingezitumia vyema ingejiweka kwenye mazingira salama zaidi itakapokuwa ugenini.

Mashabiki kwenye majukwaa hawakuwa na imani na wachezaji wao na kufanya mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kushusha lawama kwa wachezaji hao ambao mchezaji akipata mpira mashabiki wanataka aubutue mbele ambako wakati mwingine hakukuwa na mchezaji.

Hali hii iliwanyima wachezaji uhuru wa kuivujia jasho jezi ya Yanga na kufanya wacheze kwa presha kubwa ya kulitaka bao la mapema.

Mashabiki wanatakiwa kusimama nyuma ya timu muda wote bila kujali timu inapitia katika hali gani, lakini mashabiki wa Yanga hawakuwa hivi, walionekana kuishangilia timu ikiwa na mpira, lakini mpira ukiwa miguuni mwa adui mashabiki hao waliwakosoa wachezaji wao.

MC Alger kupoza mashambulizi

Muda ambao wachezaji wa Yanga na mashabiki wao wakihitaji bao la mapema bila mipango ili kuuweka mchezo kwenye himaya yao, MC Alger walilijua hili na walichokuwa wanakifanya kipindi cha kwanza ni kutuliza mashambulizi yote ya Yanga yaliyokuwa yanakwenda langoni mwao.

Kocha wa MC Alger, Moussa Kamel, alionekana kufahamu nguvu ya Yanga kwenye mashambulizi ilikuwa zaidi upande wa kulia alikocheza Hassan Ramadhan ‘Kessy’ na Simon Msuva na kujua jinsi ya kuwazima na muda mwingi wa kipindi hicho wachezaji hao wa Yanga kuonekana kukosa mipango.

Kessy, aliyecheza vyema katika pambano hilo alianza mchezo kwa kuukamia na kupoteza mipira mitatu katika dakika 10 za kipindi cha kwanza, lakini alipokuja kutulia alikuwa hatari kubwa kwenye lango la MC Alger, walionekana kucheza kwa kujihami zaidi.

Mlinzi wa kushoto wa MC Alger, Karaov Amir na mshambuliaji Awad Said aliyeingia kipindi cha pili walionekana kucheza kwa kuchelewesha muda kwa makusudi kwa kuubutua mpira nje ya uwanja mara kadhaa na kufanya mwamuzi ampe kadi ya njano Said kwa tukio hilo.

Licha ya wachezaji hao wa MC Alger, kuwa na matukio hayo, lakini wenzao Bougeuche Hajj na Nekkache Hichem walikuwa wakijiangusha ili kupoza mashambulizi ya Yanga ambao kila dakika zilivyokuwa zikienda walionekana kucheza kwa umaridadi.

Pambano la marudiano Yanga wanahitaji kuwa makini na matukio yote ya MC Alger ambao wameshawaona hapa nyumbani, hivyo wanahitaji kuzisoma mbinu walizoziona Tanzania na kujua jinsi gani wanakwenda kuwamaliza kwao Algeria.

Yanga iwachunge Chaouchi Faruzi na Goveri

Mlinda mlango wa MC Alger, Chaouchi anaweza kuwa mchezaji bora wa mechi kwa upande wa timu yake, kutokana na kuokoa mabao ya waziwazi yaliyopigwa langoni mwake.

Chaouchi, aliyewahi kuwa mlinda mlango namba moja wa timu ya taifa Algeria miaka ya nyuma alionekana kuwa kikwazo kikubwa cha Yanga kushindwa kuondoka na ushindi mnono.

Licha ya Chaouchi kuwa na sifa ya kudaka, lakini alionekana kuwapamga vyema walinzi wake kwenye mashambulizi yote ya hatari yaliyokwenda langoni.

Hata bao pekee alilolifunga kiungo mshambuliaji wa Yanga, Thaban Kamusoko lilikuwa bao la kiufundi lililopikwa vyema kwa pasi za mgongeano wa haraka na Kamusoko kupiga shuti la chinichini ambalo Chaouchi alikuja kushituka mpira uko nyavuni.

Licha ya kufungwa bao hilo, lakini Chaouchi alitoa mabao mawili ya wazi ya Obrey Chirwa na Kamusoko mwenyewe. Yanga inahitaji kujipanga upya dhidi ya mlinda mlango huyu kizingiti kama inahitaji kusonga mbele, la sivyo Chaouchi anaweza kuwa kikwazo zaidi kwenye mchezo wa marudiano ambao atacheza mbele ya mashabiki wake.

Licha ya Yanga kutakiwa kuwa makini na mlinda mlango huyo, lakini inahitaji kuwa macho na mshambuliaji Kaled aliyeonekana kuwa msumbufu kwa walinzi wa Yanga.

Kaled, alionekana kuipa kazi ya ziada safu ya ulinzi ya Yanga muda mwingi wa mchezo huo mpaka alipotolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mwingine ambaye hakuonekana kuwa na makali ya Kaled.

Mshambuliaji huyu mwenye kasi, chenga na mashuti, walinzi wa Yanga wanatakiwa kuwa nae makini katika pambano la marudiano ambalo linatarajiwa kuwa na vitu vingi vya ndani ya uwanja na nje ya uwanja.

Yanga ijiandae kisaikolojia na ilichokipata Azam Swaziland

Ndani ya uwanja mashabiki wa timu zote walipata moja ya mechi nzuri iliyomvutia kila mtazamaji aliyelipa kiingilio chake kutazama mchezo wenyewe, lakini nje ya uwanja hakukuwa na neno ‘Fair’ kwa wenyeji wetu MC Alger waliokuja na watu wao kwa ajili ya kuwashangilia.

Mpira wa Tanzania bado uko usingizini na haujui maana halisi ya neno ‘fitna’. Wanaodaiwa kuwa makomandoo wa Yanga walitumia  jazba, nguvu kuwaondoa watu waliokuja na msafara wa MC Alger kwenye maeneo ambayo walihitaji kukaa na kufanya kazi zao kwa utulivu bila kugasiwa na yeyote yule.

Kabla ya mchezo huo kuanza wanaodaiwa kuwa makomandoo hao waliwaswaga sehemu moja watu hao na kuanza kubishana nao kwa dakika kadhaa mpaka watu hao wa Algeria kufuata maelekezo waliyokuwa wakipewa.

Shida kubwa Tanzania tukiambiwa neno ‘fitna’ huwa tunajua kuwazomea wapinzani, kuwapa gari bovu au kuwanyima ushirikiano wakiuhitaji, lakini haiko hivi na neno halisi ya ‘fitna; ni kuwaona waamuzi kuzungumza nao pembeni pamoja na mambo mengine ambayo mashabiki haiwahusu.

Kwa kilichotokoea kwa wale wanaodaiwa kuwa makomandoo wa Yanga kuwafanyia fujo watu waliokuja na msafara wa MC Alger, Yanga ijiandae kisaikolojia itakapokuwa ugenini.

Azam ambao wiki kadhaa zilizopita walicheza dhidi ya Mbambane Swallows na kutupwa nje na mchezo wa kwanza uliofanyika uwanja wa Azam Complex Chamazi, tulishuhudia wanaodaiwa kuwa makomandoo wa Azam waliwaletea figisu za kitoto Mbambane, na Azam ilipoenda Swaziland kwenye mchezo wa marudiano kilichotokea kila mmoja anakijua.

Hivyo Yanga waende Algeria wakiamini fika kuna mazingira ya nje ya uwanja wakatutana nayo na kama hawajajipanga kwa umakini kazi yao kubwa walioifanya nyumbani itakuwa kazi bure.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles