Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
KLABU ya Yanga imeingia mkataba na Shirika la Bima la Taifa (NIC) wa kudhamini tuzo za mchezaji bora wa mwezi kwa kipindi cha miaka mitatu wenye thamani ya shilingi milioni 900.
Akizungumzia mkataba huo leo Oktoba 9,2023 mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Rais wa klabu hiyo, Mhandishi Hersi Said, amesema ni heshima kubwa waliyopewa na shirika hilo na makubaliano hayo yatanufaisha pande zote mbili kibiashara.
Rais huyo wa timu ya Wananchi, ameeleza kuwa kilichochangia kupata udhamini ni kutokana na uwepo wa wachezaji wenye ubora katika kikosi chao ambao wana ushawishi mkubwa ndani na nje ya uwanja.
“Tunaelewa kwa nini NIC wamechagua kufanya kazi na sisi, ni kwa sababu tuna wachezaji bora zaidi ambao huwezi kuwapata kwenye klabu nyingine. Wachezaji hawa wana ushawishi mkubwa nje na ndani ya uwanja. Ushawishi wao ni chachu ya kutangaza biashara hii ya Bima,” amesema Hersi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NIC,Elirehema Doriye, ameeleza kuwa wamefanya hivyo ili kuwapa wachezaji motisha na mashabiki sehemu ya kuzungumzia kwa kuchagua mchezaji wao bora.
“Utaratibu utakaotumika kumpata mchezaji bora wa mwezi ni jobo la benchi la ufundi kuchagua wachezaji watatu, kasha mashabiki watampigia kura mmoja,” amesema Doriye.