Na Mwandishi Wetu
BAADA ya klabu ya Yanga kupigwa faini na Shirikisho la Soka Afrika(CAF), Shirikisho la Soka nchini(TFF), limekutana na viongozi wa klabu zinazoshiriki michuano ya Kimataifa ili kufanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika michezo ya awali.
Kwa sasa timu zilizobaki katika michuano ya Kimataifa ni Biashara United, Azam FC zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika na Simba inayocheza Ligi ya Mabingwa.
TFF imekutana na klabu hizo kutokana na Kamati ya Nidhamu ya CAF kuipiga faini ya dola za Kimarekani 5,000 klabu ya Yanga kutokana na River United ya Nigeria kuripoti matukio ya kufanyiwa vurugu wakati wa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga pia imepigwa faini kutokana na kuonekana baadhi ya mashabiki uwanjani katika mchezo huo ambao ulitakiwa kuchezwa bila mashabiki.
Kwa mujibu taarifa ilitolewa na TFF leo Oktoba 12, 2021, Yanga ilipata taarifa ya malalamiko ya River United pamoja na uamuzi wa CAF kupitia shirikisho hilo lakini haikujibu.
“Pia Tanzania ilipewa onyo kutokana na kuripotiwa kwa matukio mengi kwenye vyumba vya kubadili nguo pale vilabu vyetu vinapocheza mashindano ya Kimataifa na masuala ya vipimo vya PCR vya Uviko 19.
“Klabu zinatakiwa kuheshimu na kufuata kanuni na taratibu na maelekezo ya CAF,” imesema taarifa hiyo ya TFF.