Na ZAINAB IDDY- DAR ES SALAAM
UONGOZI wa timu ya Yanga umeelekeza nguvu zake katika kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Timu hiyo iliondolewa na timu ya Simba katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo mjini Unguja, kwa mikwaju ya penalti 4-2.
Azam wametwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuifunga Simba bao 1-0 katika fainali iliyochezwa juzi katika Uwanja wa Amaan mjini humo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alisema licha ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi lakini lengo lao limetimia kwa asilimia 80.
Alisema licha ya kuhitaji kutwaa kombe hilo mwaka huu, lakini pia walikuwa wakitumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kufanya vizuri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
“Tumeshindwa kulipata Kombe la Mapinduzi lakini lengo la kutumia michuano hiyo ni kama maandalizi ya kutetea taji la ligi na michuano ya kitaifa limetimia kwa asilimia 80, hivyo hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika Ligi Kuu kuhakikisha tunapata ushindi na mwisho kuwa mabingwa,” alisema.
Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 40 huku watani wao wa jadi, Simba wakiongoza ligi kwa kuwa na pointi 44 wote wakiwa wamecheza mechi 18.
Yanga wanatarajia kucheza na timu ya Majimaji ya Songea Januari 17 mwaka huu katika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Yanga watakuwa wakicheza na Majimaji mjini humo huku wakijivunia ushindi wa mabao 3-0 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.