23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga yaishangaa APR

Yanga APRNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umeshangazwa na taarifa za wapinzani wao APR ya Rwanda kutaka kutua nchini kimya kimya kwa kuhofia kufanyiwa hujuma, lakini wamewapa tahadhari kuwa pamoja na mbinu wanazofanya kipigo ni lazima.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watarudiana na APR keshokutwa katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

APR wanadaiwa kusuka mipango ya chini chini ili waweze kutua nchini kimya kimya kwa kukwepa hujuma wanazoweza kufanyiwa na wenyeji wao kuelekea pambano la keshokutwa.

Katika mchezo wa awali uliopigwa wiki moja iliyopita Uwanja wa Amahoro, mjini Kigali, Wanajangwani hao waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo wanahitaji matokeo ya ushindi au sare yoyote ili waweze kusonga mbele.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro, alisema wamesikia taarifa za ujio wa wapinzani wao kuwa watawasili leo (jana), lakini wao kama wenyeji wao hawajui lolote jambo ambalo ni kinyume na taratibu za mashindano hayo ya kimataifa.

“Tumesikia taarifa za chini chini kuwa APR wanawasili leo (jana) kimya kimya, ndio maana tunashangaa hawajatupa taarifa sisi wenyeji wao kama zinavyoeleza taratibu za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

“Majukumu yetu ni kusimamia shughuli zote za mapokezi yao kwa kuwaandalia usafiri, hoteli na uwanja wa kufanyia mazoezi, kama sisi tulivyowapa taarifa wakati tunaenda kucheza kwao,” alisema.

Taratibu za CAF zinaeleza kuwa timu mwenyeji ina majukumu ya kuwahudumia usafiri, malazi na uwanja wa mazoezi wageni wao lakini kama hawajaridhika na huduma waliyopewa wanaweza kujigharamia wenyewe.

Wakati huo huo, viingilio vya mchezo huo vimetangazwa ambavyo vitakuwa ni shilingi 25,000 kwa watazamaji wa eneo la jukwaa kuu VIP A, VIP B na C itakuwa Sh 20,000 na upande wa viti vya orange, bluu na kijani ni shilingi elfu tano.

Alisema waamuzi kutoka visiwa vya Shelisheli wamepangwa kuchezesha mchezo huo ambapo mwamuzi wa kati ni Bernad Camile ambaye atasaidiwa na Elderick Adelaide na Gerard Pool na kamisaa ni Allister Barra kutoka Afrika Kusini.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,020FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles