22.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga yaipa kipigo Lyon

Mshambuliaji wa Yanga,Donald Ngoma(kushoto),akiwania mpira na Beki wa timu ya African Lyon, Hamad Tajiri, wakati wa mchezo  wa Ligi Kuu Vodacaom uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.
Mshambuliaji wa Yanga,Donald Ngoma(kushoto),akiwania mpira na Beki wa timu ya African Lyon, Hamad Tajiri, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Vodacaom uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.

Na THERESIA GASPER- DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Yanga, jana ilianza kasi yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo wa jana ulikuwa ni wa kwanza kwa Wanajangwani hao waliokuwa wakikabiliwa na michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya makundi.

Matokeo ya jana yaliiwezesha Yanga kujikusanyia pointi tatu na kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku vinara wanaoongoza Azam FC wakiwa na pointi nne baada ya kushuka dimbani mara mbili.

Mchezo wa jana ulianza kwa kila timu kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambapo dakika ya 18, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Deus Kaseke, aliandika bao la kuongoza, baada ya kuambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kumpiga chenga kipa, Youthe Rostand wa African Lyon na kuachia shuti lililojaa wavuni.

Yanga walizidisha mashambulizi langoni kwa Lyon ambapo dakika ya 25, Amisi Tambwe alikosa bao baada ya shuti lake kuokolewa, kabla ya Simon Msuva kujaribu kufunga kwa kichwa dakika ya 33, lakini mpira ukapaa juu ya lango.

Hata hivyo, mashambulizi ya mara kwa mara yaliwazindua wachezaji wa African Lyon ambapo dakika ya 43, Hood Mayanja alikosa bao la wazi baada ya shuti alilopiga kugonga mwamba wa lango la Yanga.

Yanga walifanikiwa kuongoza hadi mapumziko, lakini walirudi uwanjani kipindi cha pili kwa kasi ambapo dakika ya 59, Msuva alifunga bao la pili akiunganisha vema pasi ndefu iliyopigwa na Haruna Niyonzima.

Licha ya kufungwa mabao hayo, African Lyon waliendeleza jitihada za kusaka bao ambapo dakika ya 76, walicharuka na kufanya shambulizi kali kupitia kwa Tito Okello aliyepiga shuti lililopaa juu ya lango.

Dakika ya 90 ya mchezo, Juma Mahadhi aliyeingia dakika ya 77 kuchukua nafasi ya Msuva, aliifungia timu yake bao la tatu baada ya kupiga shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, timu ya Mbeya City ilifanikiwa kuichapa Toto African bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Bao hilo pekee la ushindi lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Shamte na kutinga moja kwa moja wavuni dakika ya tano ya mchezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles