23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yaibeba Azam CAF

NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
MABINGWA wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana waliibeba Azam na kuwawezesha kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani, baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yaliwafanya Yanga wakabidhiwe kombe la ubingwa huku wakiwa na machungu ya kufungwa na Azam, walioshindwa kutetea taji lao walilotwaa msimu uliopita.
Ushindi huo pia umetibua ndoto na hesabu za kocha wa Simba Mserbia, Goran Kopunovic, aliyetegemea Azam watapoteza mchezo huo na kuwarahisishia kasi ya kuchukua nafasi ya pili ili waweze kucheza Kombe la Shirikisho mwakani.
Azam wamefikisha pointi 48 ambazo haziwezi kufikiwa na Simba wenye uwezo wa kumaliza ligi hiyo kwa pointi 47, huku kila timu ikiwa imebakiwa na mechi moja.
Katika mchezo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Azam, Kipre Tchetche ndiye alikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kali dakika ya pili langoni kwa Yanga, akijaribu kupiga shuti ndani ya eneo la hatari lakini aliteleza na kuanguka.
Dakika ya tatu, Amissi Tambwe wa Yanga alijaribu kuambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kutoa pasi ndefu ambayo hata hivyo haikumfikia winga, Mrisho Ngassa aliyekuwa akiusubiri eneo la hatari ili afunge kwa urahisi.
Dakika ya saba, Tchetche alikosa bao la wazi akiwa amebaki yeye na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’, baada ya kuachia shuti kali ndani ya eneo la hatari lakini lilipaa juu ya lango.
Kiungo Mbrazil, Andrey Coutinho, aliipatia Yanga bao la kuongoza dakika ya 11, kufuatia shuti kali la mpira wa adhabu alilopiga na kutinga wavuni baada ya Tambwe kufanyiwa madhambi na Himid Mao.
Azam walisawazisha dakika ya 13 kupitia kwa Tchetche, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Yanga na kufanikiwa kuwatoka mabeki na kuachia shuti lililojaa moja kwa moja wavuni.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini wachezaji walikuwa wakianguka ovyo kutokana na utelezi, ambapo dakika ya 20 mlinzi wa Yanga, Juma Abdul alijaribu kuifungia bao timu yake kwa mpira wa krosi uliotoka nje kidogo ya lango.
Kipindi cha kwanza kilimalizika na timu zote kwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1 na kupisha kundi la mashabiki kuingia uwanjani wakiwa wameunganisha bendera ya Yanga na Azam kwa kuzifunga pamoja huku wakishangilia.
Yanga walianza kipindi cha pili kwa shambulizi kali dakika ya 50, ambapo Ngassa aliachia shuti lililopitiliza nje baada ya kuunganisha pasi safi ya Tambwe.
Dakika ya 66, Shomari Kapombe alikosa bao la wazi akiwa amebaki na kipa baada ya kupiga shuti lililotoka nje na kujikuta akianguka kutokana na utelezi uliosababishwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko ya kuwatoa Salum Telela na Pato Ngonyani na nafasi zao kuchukuliwa na Edward Charles na Kelvin Yondani, huku Azam wakimtoa Gaudence Mwaikimba na kumwingiza Didier Kavumbagu.
Mabadiliko ya Azam yaliyofanywa dakika ya 52 ya kumtoa Mwaikimba na kumwingiza Kavumbagu yalizaa matunda, baada ya mshambuliaji huyo kuiandikia bao la pili na la ushindi dakika ya 78 kwa kufanya kazi nzuri ya kukimbia na mpira kutoka katikati ya uwanja na kuachia shuti lililojaa wavuni.
Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajabu Zahir, Pato Ngonyani/Kelvin Yondani, Salum Telela/Edward Charles, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho.
Azam: Mwadini Ally, Himid Mao, Gadiel Michael, Shomari Kapombe, Agrrey Morris, Mudathir Yahya, Braison Rafael, Frank Domayo, Gaudence Mwaikimba/Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche na Brian Majwega.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles