NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga umesema hauna mpango wa kufanya usajili wa dirisha dogo kwa kuhofia kukosa wachezaji wenye sifa wanazohitaji, jambo ambalo limeungwa mkono na kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm.
Kabla ya kuanza kwa zoezi la usajili, kocha huyo raia wa Uholanzi alikuwa akisisitiza kuwa hatasajili mchezaji yeyote kutokana na kuridhishwa na viwango vya nyota waliopo kwenye kikosi hicho ambacho kinashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Dirisha la usajili wa dirisha dogo kwa klabu zinazoshiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imesimama kwa muda, lilifunguliwa rasmi juzi ambapo timu mbalimbali zinahaha kusaka wachezaji ili kuboresha vikosi vyao.
Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, aliliambia MTANZANIA jana kuwa hawafikirii kufanya usajili kwa sasa kutokana na wasiwasi kwamba watashindwa kupata wachezaji wa maana ambao wanaweza kuendana na kasi ya timu hiyo.
“Kabla ya zoezi la usajili kuanza rasmi juzi tulishaweka wazi msimamo wetu kuwa hatuna mpango wa kusajili mchezaji yeyote kwa sasa, kwani tunajua hatuwezi kupata wenye sifa na uwezo tunaowataka,” alisema.
Kauli ya katibu huyo imeungwa mkono na Pluijm, ambaye ameelezea kuridhishwa na kiwango na uwezo wa nyota wake waliosajiliwa mwanzoni mwa msimu, huku akijisifia kwamba usajili huo ulizingatia kujenga kikosi imara.
“Timu yetu inafanya vizuri tangu kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu msimu huu, hivyo sina wasiwasi na wachezaji wangu ambao naamini walikuwa ni chaguo sahihi na wanafaa kwa kuiletea mafanikio Yanga,” alisema.
Awali kwenye dirisha la usajili uliopita, Yanga ilikuwa na mipango kutaka kumuuza kiungo Mbrazil, Andrey Coutinho, ili kusaka nyota wa kimataifa ambaye atarithi nafasi yake, jambo ambalo sasa linaonekana kuyeyuka.
Hata hivyo, katika mechi za mwisho kabla ya ligi kusimama, Pluijm alikuwa akimpa nafasi kiungo huyo mwenye uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na kuonekana kiwango chake kimezidi kuimarika.