NA JESSCA NANGAWE-DAR ES SALAAM
BAADA ya beki Gadiel Michael kuendelea kuwapotezea Yanga kuhusu kusaini mkataba mpya, klabu hiyo imeachana na naye na sasa ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa beki Muharami Salum ‘Mercelo’.
Marcelo ambaye pia anaichezea timu ya
soka ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ anayetajwa kusajiliwa na Singida United kwa
mkataba wa miaka mitatu, lakini Yanga imebisha hodi klabu hiyo ya mjini Singida
na kuiomba iwape ili awe mbadala wa
Gadiel.
Mmoja wa mabosi wa Yanga ameliambia MTANZANIA, kuwa wameachana rasmi na Gadiel baada ya mchezaji huyo kuwaringia kusaini mkataba mpya, hivyo wameelekeza mawazo yao kumsajili Muharami.
“Tayari uongozi wa Yanga umeongea na bosi wa Singida United, Mwigulu Nchemba, ikiwezekana warudishiwe fedha zao za usajili wa huyo mchezaji,”alisema bosi hiyo.
Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema mjadala wa usajili wa beki huyo umefungwa na ametoa ruhusa ya mchezaji huyo kwenda popote atakapohitaji ikiwemo Simba inayotajwa kuwa mbioni kumsajili.
Kwa upande wa kocha wake Mwinyi Zahera amewataka mabosi wake kutombembeleza beki huyo na badala yake waangalie wachezaji wengine watakaokua na manufaa na mapenzi na timu yao.
Awali Yanga kupitia kwa mmoja wa mabosi wa klabu hiyo, ilisafiri hadi nchini Misri wakati Stars ikiendelea na michuano ya kombe la AFCON na kumpelekea mchezaji huyo mkataba ambapo hakusaini kutokana na kutoafikiana dau lake.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Gadiel, Jemedari Said amesema hafahamu chochote kuhusu mteja wake huyo kusajiliwa na Simba kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
“Mimi nilishafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Yanga, katibu mkuu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, baada ya Gadiel kunitaka nifanye hivyo.
“Kuna mapendekezo aliyatoa ambayo Yanga iliyakubali, baadaye walimtuma mwenyekiti wao wa usajili Misri ambapo alikutana na Gadiel lakini akamwaambia aongee na mimi, nikamwambia saini lakini hufanya hivyo.
“Hili la kusajiliwa na Simba hata mimi nasilizika tu lakini hajanishirikisha na inawezekana akawa amefanya kwani sio lazima anishirikishe,”alisema Jemedari.