25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Yanga wamshangaza Bernard Morrison

Theresia Gasper -Dar es salaam

MSHAMBULIJI wa Yanga, Benard Morrison, amecheza soka ligi za mataifa mbalimbali, lakini hakuwahi kuwaona mashabiki wenye mapenzi na timu yao kama vigogo hao wa Jangwani.

Morrison alijiunga na Yanga, wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari mwaka huu akitokea katika Klabu ya Orando Pirates ya Afrika Kusini.

Tangu alipojiunga na Yanga, mchezaji huyo raia wa Ghana amekuwa na msaada mkubwa wa kikosi hicho kiasi cha kuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki wa timu hiyo.

Alizidi kujiimarishia himaya yake Yanga, baada ya kuifungia timu hiyo bao moja na pekee  lililoipa ushindi wa 1-0 dhidi ya wapinzani wao Simba, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania  Bara, uliochezwa Machi 8, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Morrison alisema  upendo anaoonyeshwa na mashabiki wa Yanga ni mkubwa kiasi cha kumfanya ajione ana deni kubwa kwao.

“Mechi ilivyoisha mashabiki waliniita nikajua wanataka picha lakini nikashangaa naanza kupewa hela mara elfu kumi,  mara elfu tano,  nilivyoenda kuhesabu hotelini nilijikuta nina laki tano, kwa kweli nilishangaa sana.

“Siku nyingine unaweza ukatoka nje, mashabiki wanakuita na kukupa chakula,  yaani unaweza kuishi bila shida yoyote, mfano tulipokwenda Lindi kucheza na Namungo njiani mashabiki walisimama na kunizawadia kuku watatu.

“Yaani hakuna kitu kingine wanachohitaji wao zaidi ya furaha tu, hali hii imenifanya nione nina deni kubwa la kuwalipa,” alisema Morrison.

Alisema ataendelea kujituma ili kuisadia timu yake hiyo kufanya vizuri kwenye michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia.

Yanga ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 51, baada ya kushuka dimbani mara 27, ikishinda michezo 14, sare tisa na kupoteza michezo minne.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles