30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga wajipanga kukwepa hujuma

NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Yanga umefichua mikakati watakayotumia kukabiliana na hujuma za ndani na nje ya uwanja za wapinzani wao msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 38, baada ya kushuka dimbani mara 14, ikishinda12 na sare mbili, huku ikipachika mabao 27 na kufungwa nane.

Miamba hiyo ya Jangwania ambayo
jana usiku ilipangwa kuikabili Biashara United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, inapitia kipindi kigumu kutokana na kukabiliwa na ukata, licha ya kwamba imekuwa na mwenendo mzuri tangu msimu huu wa Ligi Kuu ulipoanza.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samuel Lukumay, alisema ili kuhakikisha timu yao haipepesuki na badala yake inaendelea kuwa moto, wao kama viongozi wamekuwa na utaratibu wa kaukutana na kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi kabla ya michezo yao.

“Kuiongoza Yanga ni mzigo mzito ambao unatakiwa kupambana ili kuhakikisha unapata matokeo kama yanayoonekana hivi sasa.

“Kuna changamoto nyingi lakini kubwa ni suala la ukata, huwezi kufanya jambo lolote bila fedha na mashabiki wanataka matokeo mazuri hapa ndio ukubwa wa jukumu lenyewe linapoonekana, lakini nawashukuru wanaendelea kuupa sapoti.

“Kama unavyofahamu katika ligi yetu hujuma pia zipo, sisi kama viongozi lazima tukae na kujadiliana namna ya  kuzikabili ili kutowapa mwanya wapinzani wetu kututoa kwenye reli,” alisema Lukumay na kuongeza.

“Mpira una mambo mengi ya ndani na nje ya uwanja, ifahamike kuwa hakuna mpinzani yeyote anayependa Yanga ipate mafanikio, huu ndio msingi wa kukutana na kujadili kwa lengo la kukumbushana majukumu ya kila mmoja kwa nafasi yake.”

Bosi huyo aliwataka waamuzi kuendelea kuchezesha kwa kuzingatia sheria 17 za mchezo wa soka ili timu inayoshinda ipate ushindi kwa uwezo badala ya kubebwa, akisema kinyume na hapo watakuwa sehemu ya wale wanaohujumu.

“TFF inatakiwa ifanye kazi yake kama msimamizi mkuu wa mchezo wa soka hapa nchini, waamuzi nao wazingatie sheria 17 badala ya kuingia uwanjani na matokeo yao mwisho wake wanaharibu mpira,” alisema.

Akizungumzia vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyoonekana kufanywa na wachezaji wake akiwemo Mrisho Ngassa na kusababisha kutolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu wakati wa mchezo wao na Prisons, alisema
katika mchezo wa Prisons tuliliona hilo lakini tulikaa na wachezaji wetu na kuzungumza nao, lakini pia wahusika wakae na waamuzi na kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria za mchezo wa soka ili kuepusha vurugu zisizo za lazima.”


Pia aligusia suala la usajili wa dirisha dogo kwa kusema wamepanga kuwatoa kwa mkopo wachezaji sita, ili kuwapa fursa ya kupata nafasi zaidi ya kucheza na hatimaye kuboresha viwango vyao.

“Kuna wachezaji sita tutawatoa kwa mkopo, hawa ni wale ambao hawapati nafasi ya mara kwa mara katika kikosi chetu, lengo ni wapate nafasi zaidi ya kucheza ili kuboresha viwango vyao,” alisema Lukumay bila kutaja majina ya wachezaji watakaowatoa kwa mkopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles