25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga waivamia Mgambo Tanga

MMGM00291NA OSCAR ASSENGA, TANGA

ZIKIWA zimebakia siku sita kabla ya timu ya Yanga kukipiga na Mgambo JKT ya mkoani Tanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mmoja wa vigogo wa timu hiyo ametua jijini humo wikiendi iliyopita tayari kabisa kuweka mazingira sawa ya kuibuka na ushindi.

Yanga inakabiliwa na mchezo huo mgumu utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani kwenye mwendelezo wa ligi hiyo, iliyosimama takribani mwezi mmoja na nusu kupisha michuano ya Kombe la Chalenji na mechi za mbili za timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Algeria ‘The Desert Foxes’.

MTANZANIA lilipata fursa ya kumuona kiongozi huyo wa Yanga ambaye ni Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, inaelezwa alikuja kuandaa mazingira ya timu itakapofikia ili kuzuia mianya yote ya hujuma kuelekea mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa.

Mgambo JKT yenye maskani yake Kabuku Handeni Tanga, imekuwa ikiisumbua sana Yanga na kuipasua kichwa kila wanapokutana kutokana na aina ya uchezaji wao wa kubadilika mara kwa mara kama kinyonga, jambo ambalo limeanza kuzua tahadhari kubwa kwa wapinzani wao.

Yanga ikionyesha imeupania sana mchezo huo, leo inatarajia kuingia kambini Bagamoyo, mkoani Pwani tayari kabisa kuanza maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya kuwafuata Mgambo JKT.

Wanajangwani hao wenye pointi 23 wamejipanga kushinda mchezo huo ili kuikaba koo ya Azam FC iliyoko kileleni kwa pointi 25 kama itashindwa kuzoa pointi tatu watakapocheza siku hiyo dhidi ya Simba.

Mpaka sasa wachezaji wote wa Yanga waliokuwa katika michuano ya Kombe la Chalenji wameripoti isipokuwa kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, ambaye juzi aliiongoza Rwanda kupokea kichapo cha bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali wa michuano hiyo dhidi ya Uganda.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, ameshaweka wazi kuwa mechi zake zote zilizobakia hivi sasa ni muhimu sana na amepanga kuanza vema tena ligi hiyo kwa kuichapa Mgambo JKT.

Naye Kocha wa Mgambo JKT, Bakari Shime, alisema wao wamejipanga vizuri kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo kwa sababu kikosi chao kimekamilika kila idara kuweza kuwadhibiti wapinzani wao.

“Niseme wazi kuwa hao Yanga hawatunyimi usingizi wala kutupa presha na ndio maana ninawaomba mashabiki wa soka mkoani Tanga wajitokeze kwa wingi kuja kutushangilia kwa sababu mipango yetu mikubwa ni kuibuka na ushindi,” alisema.

Shime alisema kuwa wao wanawafahamu vizuri Yanga hivyo haitakuwa kazi rahisi kwa wao kuweza kuchukua pointi tatu badala yake wajiandae kupokea virungu kutoka kwa wanajeshi hao wa kikosi cha JKT Kabuku mkoani Tanga, ambacho kinashika nafasi ya tisa kwenye msimamo ikiwa na pointi 11.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,211FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles