33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga wababe 2016

yanga 123*Wabeba ndoo mbili, Abdul, Manula, Atupele wang’ara

*Kessy, Ngassa, Nature wapamba sherehe Taifa

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga jana ilijidhihirishia kuwa ni wababe msimu huu baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la FA, kwa kuibuka na ushindi wa  mabao 3-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ubingwa huu wa FA umedhihirisha kuwa klabu hiyo ni moto wa kuotea mbali, kwani umekuja wiki moja tu baada ya kutawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2015/2016.

Yanga ilikuwa na kila sababu ya kutangaza ubabe huo kwani ilikuwa na kikosi imara kilichojaa wachezaji wenye uwezo mkubwa na vipaji vya kutosha ilisajili vema.

Uwepo wa wachezaji wa kimataifa kama Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Vicent Bossou, Amis Tambwe na wazawa Juma Abdul, Deus Kaseke, wakongwe Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan na wengine ulitosha kuifanya Yanga kubeba ndoo hizo mbili

kufuatia ushindi huo, Yanga wamefanikiwa kuondoka na kitita cha shilingi milioni 50 pamoja na kikombe hicho wakati ubingwa wa Ligi Kuu wamejishindia kiasi cha shilingi milioni 81.

Katika fainali hiyo Yanga walitumia fursa ya kumtambulisha rasmi mchezaji Hassan Kessy, waliomsajili hivi karibuni ambapo walikuwa wakimtembeza uwanjani na mashabiki wakimshangilia.

Fainali hizo zilizokuwa zimepambwa na burudani za muziki kutoka kwa msanii Juma Nature na kundi la sarakasi, ilionekana kuhudhuriwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa ambaye kwa sasa anakipiga katika timu ya Free State nchini Afrika Kusini.

Yanga ndio walikuwa wa kwanza kuandika bao la kwanza dakika ya tisa kupitia mchezaji Amis Tambwe alilofunga kwa kichwa akiunganisha pasi ya Juma Abdul, ambapo kipa wa Azam, Aishi Manula alikuwa amelihama lango lake ili kuwahi kuokoa hatari iliyokuwa inaelekezwa langoni lakini alijikuta amechelewa na mpira kutinga wavuni.

Bao hilo liliwashtua Azam ambapo dakika ya 14 John Bocco alishindwa kuitumia vema nafasi waliyoipata, hivyo kujikuta akipaisha mpira akiwa yeye na kipa baada ya kupokea pasi ya Himid Mao.

Yanga walizidisha kasi na kila wakati walikuwa wakilikaribia lango la Azam, licha ya pasi zao kushindwa kufika wavuni.

Lakini dakika ya 27 Tambwe chupuchupu aiandikie Yanga bao la pili, lakini alishindwa kuunganisha vema mpira wa faulo uliochongwa na Haruna Niyonzima hesabu zake ziligoma na mpira ule kupita juu ya lango.

Dakika ya 40 Agrey Morris alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Simon Msuva, huku dakika ya 42 Ramadhani Singano alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kelvin Yondani.

Hadi wanaenda mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0 huku Azam wakijiuliza nini cha kufanya kuweza kushinda.

Kipindi cha pili kilianza Azam wakifanya mabadiliko ambapo alitoka Bocco na nafasi yake kuchukuliwa na Didier Kavumbagu.

Yanga iliandika bao la pili kwani dakika ya 47 mfungaji akiwaTambwe kwa shuti akiunganisha vema krosi iliyochongwa na Simon Msuva.

Mabadiliko ya Azam yalizaa matunda dakika ya 49 kwa kuandika bao la kwanza kupitia Kavumbagu, aliyefunga kwa kichwa akitumia vema uzembe wa mabeki wa Yanga.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika ya 58 kwa kumtoa Oscar Joshua aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi Haji, pia ilifanya dakika ya 68 kwa kumpumzisha Niyonzima na kuingia Mbuyu Twite, huku dakika ya 63 Azam walimtoa Mudathir Yahya na nafasi yake kuzibwa na Frank Domayo.

Donald Ngoma dakika ya 71 alijitengenezea nafasi nzuri ya kuandika bao la tatu, aliwapiga chenga ya kuvutia mabeki wa Azam lakini alijikuta akishindwa kufanya maamuzi ya haraka, alipolikaribia lango na kuamua kumpa pasi JumaAbdul ambaye alipiga shuti lililodakwa na Manula.

Dakika ya 72 Abdallah Henry alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Msuva.

Deus Kaseke aliwaongezea furaha mashabiki wa Yanga dakika ya 81 baada ya kuandika bao la tatu, aliachia shuti kali lililomshinda kipa Manula na kutikisa nyavu za Azam akimalizia pasi safi ya Thabani Kamusoko.

Azam waliendelea kufanya mabadiliko ili waongeze nguvu ambapo dakika ya 83 alitoka Agrey Morris na nafasi yake kuchukuliwa na Shabani Iddy, wakati Yanga walimtoa Bossou dakika ya 87 na kuingia Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Baada ya kumalizika michuano hiyo, Juma Abdul wa Yanga alitangazwa kuwa mchezaji bora, kipa bora  akiwa Aishi Manula wa Azam FC wakati mfungaji bora akiwa Atupele Green wa Ndanda FC.

 

Kikosi Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Donald Ngoma, Amis Tambwe, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles