24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA VS SIMBA Ukizubaa umeliwa

mashabiki yanga simbaNA ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

UKIZUBAA umeliwa! Hivyo ndivyo tunavyoweza kusema pale watani wa jadi Yanga na Simba watakapokutana leo katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huu ni mchezo ambao kila shabiki wa soka  anatamani kuuona ambao utaanza saa 10:00 jioni katika uwanja huo unaochukua watazamaji 60,000.

Mchezo huo ndio utakaotoa taswira ya mbio za ubingwa msimu huu, ambao unashikiliwa na Yanga kwa sasa.

Yanga ambao ndio wenyeji wa mchezo huo  wanaingia uwanjani wakiwa na pointi 43 katika michezo 18 wakiwa nyuma ya Simba wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi 45 baada ya kucheza michezo 19 .

Mchezo huo unatabiriwa kuwa mgumu baada ya kila timu kuonekana kuwa vizuri kwenye idara zote na utachezeshwa na mwamuzi, Jonesia Rukyaa kutoka Kagera, akisaidiwa na mwamuzi Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha) wote wakiwa waamuzi wenye beji za Fifa, mwamuzi wa akiba Elly Sasii (Dar) na Kamisaa wa mchezo huo atakua Khalid Bitebo (Mwanza).

Kwa upande wa Simba tangu kukabidhiwa kikosi kocha Jackson Mayanja, kimeonekana kurejea katika ubora wake kwani imeweza kupata matokeo ya ushindi katika michezo mitano mfululizo nyumbani na ugenini.

Licha ya hali hiyo, inatabiriwa kuwa ni mechi ya kisasi kwa Simba kwani mzunguko wa kwanza walikubali kipigo cha mabao 2-0, hivyo Wekundu hao wa Msimbazi wanahitaji kushinda ili kurejesha heshima yao.

Ili kurejesha heshima hiyo, Simba baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United mkoani Shinyanga, iliamua kujichimbia katika milima ya Uluguru mkoani Morogoro ambako wameamini ni sehemu tulivu kwao.

Mbali na kurejesha heshima mbele ya Yanga, lakini pia Simba itaingia uwanjani ikiwa inahitaji ushindi wa aina yoyote ili iweze kujiimarisha kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliokaa kwa mara ya kwanza tangu kuanza msimu huu.

Wakati Simba wakijichimbia mkoani Morogoro, Yanga nao waliamua kulitosa Jiji la Dar es Salaam na kwenda kufuata marashi ya karafuu huko Pemba na kuweka kambi.

Vijana hao wa Hans van der Pluijm, waliamua  kwenda Pemba baada ya kambi yao ya mwisho kujiandaa na watani zao  kuwapa matunda ya ushindi wa mabao 2-0.

Yanga wataingia uwanjani wakiwa wametokea Mauritius walipokwenda kucheza mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Licha ya hivi karibuni nusura Yanga wapoteane baada ya kujikuta wakipoteza mchezo kwa kufungwa na Coastal Union mabao 2-1 na kuambulia sare ya mabao 2-2 na Tanzania Prisons, lakini itahitaji ushindi mbele ya Simba ili kulinda heshima yao pamoja na kukwea kileleni mwa ligi hiyo.

Mbali na uwezo wa vikosi hivyo viwili msimu huu, rekodi zinaonyesha timu hizo zilizoanzishwa mwaka 1935 (Yanga) na mwaka 1936 (Simba), zimekutana mara 80 huku Wanajangwani ndio wanaoongoza kwa kuwafunga Wekundu wa Msimbazi katika michezo ya ligi.

Yanga imefanikiwa kuwa wababe mbele ya watani zao mara 30, huku Simba ikiibuka washindi mara 23 na mara 27 zikitoka sare.

Ukiacha hayo yote, kivutio kikubwa kwenye mtanange huo ni washambuliaji wa kimataifa wa timu hizo, Amissi Tambwe wa Yanga (Mrundi) pamoja na Hamis Kiiza kutoka Simba (Mganda), hiyo inatokana na jinsi walivyoanza vizuri kwenye mechi zilizopita msimu huu, ukizingatia pia wote wapo kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu.

Mpaka sasa Kiiza ana mabao 16 wakati Tambwe ametikisa nyavu mara 14 huku kila mmoja akifanikiwa kupiga ‘hat trick’.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo ni pamoja na Mgambo Shooting itakayokuwa katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga, kuwakaribisha Tanzania Prisons  kutoka Mbeya, wakati  Stand United wakiwakaribisha JKT Ruvu katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Azam wao watakuwa ugenini mkoani Mbeya kucheza na Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine, wakati Toto Africans watawakaribisha Kagera Sugar katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Tiketi za mchezo huo zimeanza kuuzwa jana saa 2 asubuhi katika vituo 10 mbalimbali vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Vituo vinavyotumika kuuza tiketi ni ofisi za TFF – Karume, Buguruni Oilcom, Ubungo Oilcom, Uwanja wa Taifa Temeke, Mavuno House – Posta, Dar Live Mbagala, Breakpoint – Kinondoni, Kidongo Chekundu – Mnazi Mmoja, Mwenge na Kivukoni Ferry.

Kiingilio cha juu cha mchezo huo ni Sh 30,000 kwa VIP A, Sh 20,000 VIP B na C, Sh 10,000 kwa viti vya rangi ya machungwa na Sh 7,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani na milango itakuwa wazi kuanzia saa 5 asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles