29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA, SINGIDA UNITED MOTO KUWAKA TENA SHIRIKISHO

 

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM


TIMU ya Yanga ina kibarua kizito cha kuhakikisha inaichapa Singida United ili kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Timu hizo zitakutana katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya kwanza ya michuano hiyo, baada ya droo iliyochezeshwa jijini Dar es Salaam jana.

Timu nane zilizotinga  robo fainali ya michuano hiyo ni Yanga, Stand United, Azam FC, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar, Singida United na  Njombe Mji.

Mchezo huo utapigwa mwishoni mwa mwezi huu wa Machi kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Huo utakuwa mchezo wa nne timu hizo kukutana tangu Singida ilipofuzu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Awali, timu hizo zilikutana katika Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi na mchezo mmoja wa kirafiki.

Yanga ilishinda mara moja, ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki, huku mara mbili zilitoka sare, suluhu katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Namfua na sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi.

Kimsingi makocha wa timu hizo, George Lwandamina na Hans van der Pluijm wa Singida United, kila mmoja anaujua ubora na udhaifu wa mpinzani wake.

Lakini Pluijm ndiye mwenye faida kubwa zaidi ya Lwandamina, kwani anaifahamu sawa sawa Yanga kwa kuwa aliwahi kuifundisha kwa mafanikio makubwa akitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu, kabla ya kujiunga na Singida United.

Kulingana na droo hiyo, Prisons itaumana na JKT Tanzania katika mchezo wa robo fainali ya pili kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Azam FC itaikaribisha Mtibwa Sugar  katika mchezo wa robo fainali ya tatu kwenye Uwanja wa Azam Complex, wakati  Stand United itatunishiana msuli na Njombe Mji katika mchezo wa robo fainali ya nne kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mshindi wa robo fainali ya kwanza kati ya Singida United na Yanga atakuwa nyumbani kusubiri mbabe kati ya Prisons na JKT Tanzania kwa mchezo wa nusu fainali.

Nusu fainali ya pili itahusu mbabe kati ya Azam na Mtibwa dhidi ya mshindi wa mchezo kati ya Stand United na Njombe Mji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles