30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Simba, Azam mawindoni

hans-pluijmNA WAANDISHI WETU

VIGOGO wa soka nchini timu za Simba, Yanga na Azam, leo zinatarajiwa kushuka dimbani katika viwanja tofauti kuchuana vikali katika mechi za mwendelezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), iliyoanza kutimua vumbi Jumamosi iliyopita.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga, wapo kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku wapinzani wao, Simba na Azam wakifuatia jambo linalofanya ushindani wa mechi za leo kuwa mkubwa kutokana na timu hizo kuwa kwenye vita ya ubingwa.

Yanga itabaki kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuwakaribisha maafande wa Tanzania Prisons, ambao walianza vibaya Ligi Kuu kwa kupata kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Azam Jumamosi iliyopita.

Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Hans van Pluijm, aliliambia MTANZANIA jana kuwa wamejiandaa vya kutosha kwa mchezo huo na anafahamu vizuri staili ya uchezaji wanayoitumia maafande wa Tanzania Prisons.

“Jambo la msingi ni wachezaji kucheza kwa kujituma uwanjani na kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo huo kuanzia mwanzo hadi mwisho kuhakikisha wanaibuka na ushindi kama walivyofanya awali kwa Coastal Union,” alisema.

Simba walioichapa African Sports bao 1-0 katika mechi ya awali, wataendelea kuwa ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kumenyana na Mgambo JKT ya huko.

Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, amejihakikishia ushindi mnono dhidi ya maafande hao huku akionekana kuwapa mazoezi makali wachezaji wake, akiwataka kupiga pasi 100 bila kupoteza kwa adui katika mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Disuza jana.

Jambo linalomnyima raha Kerr ni kitendo cha kukutana na Mgambo huku akiwa hafahamu mfumo unaotumiwa na Kocha wa Mgambo, Bakari Shime, lakini amejipa moyo kwamba watatumia uzoefu kwa kupata kikosi bora cha ushindi.

Katika mchezo huo Simba watamkosa mshambuliaji wao wa kulipwa, Daniel Lyanga, kutokana na kukosa hati ya uhamisho wake wa kimataifa (ITC) kutoka timu yake ya awali ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao bado hawajaituma.

Kwa upande wake kocha Shime wa Mgambo Shooting, alisema kamwe Simba haiwezi kuvunja mwiko kupata ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani huku akidai kikosi chake kipo fiti kuwavaa wapinzani wao.

Azam iliyosafiri hadi mkoani Shinyanga itakuwa ikisaka pointi tatu nyingine kwa kuivaa Stand United ya huko, kocha mkuu wake, Stewart Hall, amesema ataendeleza wimbi la ushindi kwenye mechi hiyo na nyingine zinazofuata.

Wakati Azam ikianza vema mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo kwa kuichapa Tanzania Prisons mabao 2-1, Stand United ilichapwa nyumbani na Mtibwa Sugar bao 1-0 nyumbani.

“Katika mechi yetu na Prisons tungeshinda zaidi ya mabao manne au matano lakini washambuliaji walipoteza nafasi nyingi, hata hivyo, katika kipindi hiki tutawekana sawa kuhakikisha tunakamilisha malengo yetu kwa kushinda dhidi ya Stand United na mechi zinazokuja,” alisema.

Katika mechi nyingine, Mtibwa Sugar iliyoanza kwa ushindi dhidi ya Stand United, watakuwa ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuchuana na Toto African, mchezo ambao umetabiriwa ugumu na kocha wake, Mecky Mexime. Toto nayo ilipata ushindi huo walipoivaa Mwadui.

Majimaji watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji Songea huku Mbeya City wakitarajiwa kufuta machungu ya kufungwa kwa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Ndanda FC watawakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, baada ya kujeruhiwa na Yanga kwa kufungwa mabao 2-0 Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

HABARI HII IMEANDIKWA NA ONESMO KAPINGA, TANGA NA JUDITH PETER, MWALI IBRAHIM, ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles