Yanga kujipima na Coastal Union J’pili

0
1035
Kiungo wa Yanga, Mapinduzi Balama(kushoto), akimtoka Ayub Lyanga wa Coastal Union, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda bao 1-0, lililofungwa na kiungo, Abdulaziz Makame. Picha na Loveness Benard.

THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union Jumapili hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ikiwa ni moja ya mipango ya kujiweka fiti katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi hicho kilirejea juzi jijini Dar es Salaam na kuendelea kufanya mazoezi katika Uwanja wa Polisi uliopo Kurasiji, jijini hapa.

Yanga ilikuwa mkoani Mtwara ambao walicheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC na kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Timu hiyo pia ilicheza michezo miwili ya kirafiki huko Mtwara kabla ya kurejea Dar es Salaam, ikiichapa Nanyumbu Combine mabao 5-0, kabla ya kupokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mkuti ya Ligi Daraja la Pili.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, alisema baada ya kurejea Dar es Salaam, wachezaji wanatarajia kuendelea na mazoezi ili kuendelea kujiweka fiti.

“Kocha mkuu anataka mchezo mwingine wa kirafiki ambako tutacheza dhidi ya Coastal Union, kwani awali ilikuwa tucheze na Ruvu Shooting, lakini ilishindana hivyo kwa sasa tutaangalia nyingine,” alisema.

Bumbuli alisema wachezaji wote wapo fiti na kila mmoja anaonyesha morali ya juu ambako benchi la ufundi litatumia muda huu kuhakikisha wanayafanyia kazi baadhi ya makosa yaliyojitokeza nyuma.

Yanga inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi 10 kati ya mechi tano walizocheza, wakishinda michezo mitatu na kutoa sare moja, huku wakipoteza mmoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here