27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga kufunga mjadala Kanda ya Ziwa

Winfrida Mtoi

TIMU ya Yanga inatarajia kushuka dimbani leo kuivaa Gwambina FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Gwambina Complex, uliopo Misungwi, Mwanza.

Mchezo huo utakuwa wa tatu mfululizo kwa Wanajangwani hao kucheza wakiwa Kanda ya Ziwa baada ya kufanikiwa kushinda mbili zilizopita.

Yanga ilikwenda jijini Mwanza wiki iliyopita  ambako ilianza kucheza na KMC na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1  Uwanja wa CCM Kirumba, baadaye kuelekea Mara kukipiga na Biashara United na kuifunga 1-0 kwenye Dimba la Karume.

Ushindi wa michezo hiyo miwili mfululizo ugenini, umeifanya Yanga kukaa nafasi ya pili ikifikisha alama 22 zilizotokana na mechi nane, pointi sawa na Azam FC inayoongoza baada kushuka dimbani mara tisa.

Endapo Wanajangwani hao watafanikiwa kuchukua alama tatu kwa Gwambina, watakuwa wamekamilisha malengo yao ya kuchukua pointi tisa Kanda ya Ziwa na itaishusha Azam kileleni.

Kutokana na kiwango cha wachezaji wa Yanga walichokionesha katika michezo miwili iliyopita kwa kuwa na hamu ya kushinda, huenda ikaongezeka leo ili kufikia malengo yao.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa vuta ni kuvute kutokana na Gwambina kuongozwa na Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi, Mwinyi Zahera ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Wanajangwani hao.

Gwambina inakutana na Yanga ikiwa imetoka kuchapwa mabao 3-0 nyumbani na KMC, hivyo itakuwa na hasira za kutaka kulipa kisasi.

Pia mchezo huo utatoa picha ya Yanga kuelekea katika mechi na watani wao wa jadi, Simba unatarajiwa kupigwa wikiendi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Matarajio ya Wanayanga wengi ni kuona Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Cedric Kaze, amefanyia marekebisho katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikishindwa kutumia vizuri nafasi zinazotengenezwa.

Akizungumzia mchezo huo, Kaze alisema anaendelea kufanyia kazi mambo mbalimbali ndani ya kikosi chaka, lakini lengo la kwanza  wanaloingia nalo uwanjani ni kupata pointi tatu.

“Michezo ya ugenini ni migumu siku zote, ukipata alama tatu ni jambo kubwa, wachezaji wangu wamefanya kazi nzuri katika mechi zilizopita, tunaamini hata mchezo na Gwambina tutashinda,” alisema.

Alisema aliifuatilia Gwambina katika mechi zake chache, anajua ni aina gani ya soka wanalocheza lakini ataingia na mbinu tofauti kwa sababu muda wowote timu inabadilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles