NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TIMU ya Yanga inatarajia kucheza na JKT Ruvu kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Jumatano ikitarajiwa kuwafuata wapinzani wao timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius, kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van der Pluijm, amesema maandalizi yao yapo vizuri na yanatosha kuiwezesha kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao hao Jumamosi katika Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe.
Yanga ambao wapo kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 40, watakuwa wanahitaji ushindi dhidi ya JKT Ruvu ili iweze kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi hiyo kabla ya kuelekea Mauritius.
Mbali na Yanga, michezo mingine ya ligi hiyo itakayoendelea kesho ni Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati Ndanda FC watawakaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Leo kutakuwa na mchezo mmoja katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kati ya wenyeji African Sports dhidi ya Stand United ya Shinyanga.
Katika mwendelezo wa ligi hiyo kesho, Kagera Sugar watacheza dhidi ya Simba SC katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Azam FC watawakaribisha Mwadui FC katika Uwanja wa Chamazi, Majimaji dhidi ya Mgambo Uwanja wa Majimaji mjini Songea na Toto Africans watawakaribisha Coastal Union katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.