26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

YANGA INAWALA TU

Mwandishi Wetu, Mwanza

TIMU ya Yanga jana iliendeleza wimbi la ushindi, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1dhidi ya Alliance, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara,  uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Yanga, tangu Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles  Mkwasa alipokabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo, akirithi mikoba ya Mwinyi Zahera aliyetimuliwa.

Mkwasa aliiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda, akaichapa mabao 3-2 JKT Tanzania kabla ya jana kuitungua Alliance.

Kutokana na ushindi wa jana, Yanga imefikisha pointi 16 na kukamata nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi hiyo,  baada ya kucheza michezo saba, ikishinda mitano, sare moja na kupoteza mmoja.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Patrick Sibomana dakika ya 25 na David Molinga dakika ya 71, huku lile la Alliance ya 55.

Mabao yote ya jana yalifungwa kwa mashuti.

Mchezo ulianza kwa Yanga kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Alliance.

Dakika ya kwanza, mpira wa kichwa uliopigwa na Molinga  akiunganisha krosi ya Juma Abdul ulitoka nje kidogo ya lango la Alliance.

Deus Kaseke ilibaki kidogo aiandikie Yanga bao la kuongoza dakika ya tisa, baada ya kupiga krosi lakini mpira ulipita pembeni ya goli.

Alliance ilizinduka dakika ya 15, ambapo David Richard alijikuta akishindwa kufanya uamuzi sahihi akiwa ndani ya 18, akiwa amebaki yeye na mlinda mlango wa Yanga, Farouk Shikalo, baada ya mkwaju wake kutoka nje.

Sibomana aliwainua mashabiki wa Yanga dakika ya 25, baada ya kufunga bao kwa shuti akiwa ndani ya 18, akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na beki wa Alliance katika harakati za kuokoa.

Dakika ya 35, Molinga alijikuta akishindwa kufanya uamuzi sahihi, akiwa ndani ya 18, huku akiangaliana na kipa wa Alliance Adrew Ntala, ambapo alipiga mkwaju dhaifu uliodakwa.

Kipindi cha kwanza kilimazika Yanga ikiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko, alitoka Juma Balinya na kuingia Sadney Urikhob.

Dakika ya 55, Mwangi aliisawazishia Alliance baada ya kutumia vizuri uzembe wa mabeki wa Yanga kuchelea kuondosha mpira kwenye  eneo lao.

Bao hilo liliizindua Yanga na kufanya shambulizi kali dakika ya 58, ambapo mpira wa kichwa uliopigwa na Kaseke akiunganisha krosi ya Abdul ulipaa juu ya lango la Alliance.

Mashambulizi ya Yanga yalizaa matunda dakika ya 71, baada ya Molinga kupachika bao la pili akiunganisha vema krosi ya Kaseke.

Alliance ilijibu shambulizi dakika ya 74, ambapo mkwaju wa Michael Chinedu ulipanguliwa na Shikalo.

Yanga ilikaribia kuandika bao dakika ya 85, lakini mpira wa kichwa uliopigwa na Molinga ulipaa juu ya lango la Alliance.

Dakika 90 zilikamilika  kwa Yanga kutakata kwa ushindi wa mabao 2-1.

Katika mchezo mwingine uliochezwa dimba la Kaitaba mkoani  Kagera, wenyeji Kagera Sugar walilazimishwa suluhu na Ndanda FC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles