31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga imepata ilichostahili, tatizo liko wapi?

TUTAKUWA tunadanganyana tu kuulizana kilichoiponza Yanga katika mchezo wa juzi. Ilikuwa sahihi kabisa kupoteza mchezo ule dhidi ya River United FC iliyotua nchini ikitokea jijini Lagos, Nigeria.

Hakuna kilichotokea kwa bahati mbaya kwa dakika zote 90 za mchezo ule wa hatua ya awali ya michuano mikongwe Afrika, Ligi ya Mabingwa. Na badala yake, zilikuwapo sababu za wawakilishi hao wa Tanzania kuangukia pua kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Wanigeria hao.

Ikumbukwe, mtanange huo ulichezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kuishuhudia River United ikipata bao pekee katika dakika ya 50, mfungaji akiwa ni nahodha wake, Omoduemuke Mosses.

Wachezaji Yanga wamepotezaje mchezo?

Hakuna timu dhaifu kwenye michuano hii lakini River United FC haikuwa na ukubwa mbele ya Yanga. Katika mchezo huo, hasa kipindi cha kwanza, Yanga ilikosa nafasi nyingi za wazi, ambazo kama zingetumika, basi River United FC isingekuwa na pakutokea.

Kwa nyakati tofauti za mechi hiyo iliyochezwa bila mashabiki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kukosa umakini kuliwafanya Yacouba Sogne, Herritier Makambo, Feisal Salum na Jesus Muloko washindwe kupachika mabao ya wazi.

Mathalan, sekunde 30 tu baada ya mchezo kuanza, Sogne angeweza kuifungia Yanga lakini alishindwa kulazimisha kuingia kwenye boksi na hatimaye kutoa nje pasi iliyomfikia Zawadi Mauya aliyepiga shuti lililopaa.

Katika dakika ya 20, Aduyum Salehe naye angeweza kuifungia Yanga bao la kuongoza lakini shuti lake lilikosa macho na kuelekea nje ya lango la River United.  Ni kama Makambo alivyokosa bao la wazi dakika ya 25.

Aidha, dakika ya 27 ilimshuhudia Sogne akiwa peke yake kwenye boksi la wapinzani lakini alikurupuka kupiga mpira wa kichwa uliotoka nje ya lango. Makosa ya aina hiyo yalijirudia dakika ya 65, safari hii akiwa ni Feisal Salum aliyekuwa peke yake lakini akafumua shuti lililopaa juu ya lango.

Ni kweli River United wangeweza kushinda mechi ile lakini ulikuwa ni uzembe mkubwa wa safu ya ushambuliaji ya Yanga kuondoka uwanjani wakiwa hawajaziona nyavu za wapinzani wao hao.

Viongozi watabeba lawama?

Mchezo ule ulikuwa ni kama wa kushitukiza kwa Yanga. Hakuna ubishi kuwa Yanga haikuwa na maandalizi ya kutosha kuelekea dakika 90 za

kuikabili River United. Ni kosa kubwa lililofanywa na viongozi kuifanya timu ikose ‘pre-season’ ya kueleweka, hasa ikizingatiwa kuwa inakabiliwa na michuano ya kimataifa.

Yanga, licha ya kikosi chake kujaza wachezaji wengi wapya, wengi walitarajia kuona ikitafutiwa mechi nyingi, tena ngumu, za kujenga muunganiko (chemistry), jambo ambalo halikutokea kwa kipindi chote cha maandalizi.

Wakati timu zingine zikijiandaa vilivyo, mathalan Zesco iliyokaa kambi kwa miezi kadhaa kujiandaa na msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, Yanga ni kama ilikuwa ‘bize’ na matukio ya nje ya uwanja, kwa maana ya kuiandaa Siku ya Mwanachi.

Ni kweli iliweka kambi nchini Morocco lakini cha kushangaza ni kwamba ilikaa huko kwa siku tano pekee, achilia mbali kutopata hata mchezo mmoja wa kujipima nguvu.

Ni kusema, mechi pekee iliyokuwa na uzito wa kimashindano kwa kikosi cha Yanga ni ile ya kufungwa mabao 2-1 na vigogo wa soka la Zambia, Zesco United, katika kilele cha Siku ya Mwananchi.

Kutokana na usajili mzuri uliofanywa kwa kuzingatia mapungufu ya msimu uliopita, huenda tusingeyashuhudia yaliyotokea juzi endapo Yanga ingepata mechi zaidi ya tano za aina ile. 

Kocha Nabi naye vipi?

Hakuna namna ambayo benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha Nasredeen Nabi linaweza kuepuka lawama kwa kile kilichotokea katika mchezo wa juzi dhidi ya River United.

Huenda ni woga au sababu zingine, lakini ilishangaza kuona kocha Nabi akishindwa kumwita kwenye benchi la wachezaji wa akiba winga wa kimataifa wa DRC, Jesus Muloko.

Mbinu zake zilishindwa kuzaa matunda upande wa kulia, kisha akahamia kushoto ambako pia hakuweza kuwa tatizo kwa River United. Kwanini alimaliza dakika 90, huku benchi la wachezaji wa akiba likiwa na Deus Kaseke na Farid Mussa?

Aidha, unaweza kuhoji uwezo wa kocha Nabi katika kufanya mabadiliko kwa namna alivyochelewa kumwita benchi Sogne, licha ya kwamba winga huyo alionekana kutokuwa mchezoni, hasa katikati ya mchezo.

Labda ungetarajia kuona Saido Ntibazonkiza akiingia mapema lakini hilo lilifanyika muda ukiwa umeshakwenda zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles