29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

YANGA ENDELEENI KUCHIMBA DAWA GARI LINAWAACHA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


KUNA misemo mingi ya wahenga wakisisitiza kuwa binadamu hujifunza kutokana na makosa ya awali ili aweze kufikia malengo na mafanikio aliyokusudia.

Lakini mara nyingi klabu ya soka ya Yanga, imekuwa tofauti na misemo hiyo kwa kufanya makosa yanayojirudia wanapokuwa katika michuano ya kimataifa.

Na ndiyo sababu kubwa inayosababisha mashabiki wengi wa Yanga kushindwa kuielewa kauli ya utetezi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa  ya kwamba Yanga bado wanaendelea kujifunza, baada ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia.

Mkwasa licha ya kuwa Katibu alikuwa  miongoni mwa wachezaji wakongwe waliowahi kucheza katika timu hiyo kabla ya kuifundisha, hivyo kauli yake inaonekana kuwa na ukakasi katika masikio ya mashabiki wa timu hiyo kutokana na Yanga kuwa na miaka mingi ya kujifunza tangu kuanzishwa kwake.

Ikumbukwe Yanga ina zaidi ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwake na ndiyo klabu pekee Tanzania iliyoshiriki mara nyingi michuano ya kimataifa ikifuatiwa na Simba.

Kwa maana hiyo ni vigumu mashabiki wa timu hiyo kuwaaminisha kuwa bado wanaendelea kujifunza kwa kuzidi kufanya vibaya hata kwa timu vibonde.

Wanajangwani hao Machi 11 mwaka huu, walitolewa na Zanaco ya Zambia kwa bao la ugenini baada ya kumaliza kufungana bao 1-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kupata suluhu kwenye  mchezo wa marudiano uliochezwa nchini Zambia.

Baada ya kutolewa katika michuano hiyo, Yanga sasa wanatarajia kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo wamepangwa na timu ya Mouloudia Club d’Alger maarufu kama MC Alger ya Algeria katika mchujo wa kuwania hatua ya makundi.

Lakini Yanga wamekuwa na rekodi nzuri ya kushiriki michuano ya kimataifa bila mafanikio kwa kipindi kirefu, hususani tangu mahasimu wao Simba wamekuwa hawafanyi vizuri.

Kipindi chote hicho Yanga wamekuwa wakijisifu kuliwakilisha Taifa kimataifa hata wakifanya vibaya hujitetea kwamba msimu ujao wanaendelea kujifunza na kuboresha walipokosea.

Katika hilo, klabu ya Yanga imeonekana kufanya mabadiliko mbalimbali ikiwamo kusajili makocha wapya pamoja na wachezaji wenye sifa mbalimbali za kimataifa, lakini wamekuwa wakiambulia patupu.

Ugonjwa wa kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo umekuwa ukiwasumbua kwa muda mrefu huku wasijue tiba halisi na matokeo yake wakiishia kunyoosheana vidole wakitafuta mchawi.

Matokeo mabaya ya Yanga katika michuano ya kimataifa yametokea katika wakati tofauti yaani wakiwa na fedha na walipotetereka kiuchumi, hivyo ni ugonjwa wa kihistoria.

Msimu huu tumaini kubwa la mashabiki wa timu hiyo ni kwa kocha mpya Mzambia, George Lwandamina, ambaye tayari ameonesha dalili ya kuzidiwa na ukubwa wa matarajio ya mashabiki wa timu hiyo.

Kwani tangu achukue mikoba ya kuifundisha timu hiyo kutoka mikononi mwa Hans van der Pluijm, Lwandamina hajafanya vizuri si Ligi Kuu Tanzania Bara wala  Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo ametolewa na kudondokea Kombe la Shirikisho ambapo hata huko hakuna matumaini yoyote ya kufanya vizuri.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles