NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
HAKUNA mbabe, unaweza kusema hivyo baada ya klabu ya Yanga na Coastal Union kuamua yaishe kwa kupokezana Uwanja wa Gombani, Chake chake Pemba kwa ajili ya kufanya maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajia kuanza Septemba 20.
Timu hizo zote zimejikuta zikiwa na vibali vya kuutumia uwanja huo kwa ajili ya maandalizi hayo, ambapo kila mmoja alishindwa kumuachia mwenzake hadi walipoamua kuafikiana.
Kutokana na kuafikiana huko, Coast wataanza mazoezi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa mbili na kuwapisha Yanga ambayo imeamua kuanza mazoezi yake ya asubuhi kuanzia saa 2 hadi saa 5, wakati mazoezi ya jioni Yanga wataanza saa 9 hadi 10 na Coastal wao wakianza saa 10 hadi saa 12.
Kwa mujibu wa msemaji wa Coastal Union, Oscar Assenga, alisema kutokana na ratiba hiyo kumekuwa hakuna muingiliano kati yao na Yanga, huku kila timu ikifanya mazoezi kwa uhuru.
“Ratiba yetu ya mazoezi imeanza vizuri, tangu jana (juzi) tulipowasili kisiwani na kuanza mazoezi jioni bila programu zetu kuingiliana,” alisema.
Alisema wachezaji wao wote wapo katika kambi hiyo sambamba na benchi la ufundi, ambapo kambi hiyo itadumu hadi kukaribia kuanza kwa Ligi Kuu, huku wakipanga kucheza mechi nne za kirafiki.
Aliongeza kuwa kwa upande wa usajili lolote linaweza kutokea, kwani muda wa usajili umeongezwa hivyo uongozi unaweza kuamua kumuongeza mchezaji yeyote.