Yanga: Coastal ilikuwa lazima wapigwe

0
642

Theresia Gasper -Dar es salaam

KOCHA msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, amesema ilikuwa lazima wapate ushindi katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union uliochezwa juzi kutokana na rekodi ya matokeo ya nyuma.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Yanga ilishinda bao 1-0, shujaa wao akiwa ni kiungo Abdulaziz Makame aliyezifumania nyavu za Coastal Union kwa kichwa, baada ya kona iliyochongwa na Mrisho Ngassa na mpira kutua kichwani kwa Ally Ally kabla ya kumfikia mfungaji.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwandila alisema haikuwa kazi rahisi kupata matokeo kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo katika mchezo huo.

“Kushinda mchezo wa leo (juzi) lilikuwa ni lengo letu kwani hatukuweza kupata matokeo mazuri katika michezo miwili ya nyuma baada ya mmoja kufungwa na mwingine kutoa sare,” alisema.

Alisema waliona kasoro kadhaa, hivyo wataendelea kuzifanyia kazi waendelee kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao.

Mwandila alisema wanaamini watakaa vizuri na kuonyesha makali yao kama ilivyokuwa awali.

Upande wake, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, alisema vijana wake walipambana lakini hata hivyo bahati haikuwa upande wao.

“Nafahamu tumecheza na Yanga timu kubwa ambayo muda wowote inaweza ikapata matokeo, tulipata nafasi nyingi lakini hatukuweza kuzitumia,” alisema.

Yanga kwa sasa inashika nafasi ya 14 ikijikusanyia pointi nne kutokana na michezo mitatu waliyocheza, wakishinda mmoja na kutoa sare moja, huku wakipoteza mmoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here