30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Azam waamue sasa kimataifa

CCNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

MATARAJIO makubwa ya Watanzania ni kuona siku moja timu zao zinazopata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa zinafanikiwa.

Hatua hiyo inaambatana na imani kwamba hakuna kinachoshindikana kwenye soka, kwa kuwa mwamuzi wa mwisho ni dakika 90.

Tanzania kwa sasa inawakilishwa na Yanga na Azam katika michuano ya kimataifa, Azam imeinyakua nafasi hiyo kwa Simba baada ya kuleta mapinduzi makubwa katika soka la Tanzania, kwani awali ilikua ni Yanga na Simba ndio zinapata nafasi hiyo.

Yanga ilianza vema kampeni zake visiwa vya Port Louis nchini Mauritius, ambapo bao pekee la mshambuliaji raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma, lilitosha kuwapa ushindi dhidi ya wenyeji wao, Cercle de Joachim.

Uimara wa kikosi cha Yanga uliweza kuendeleza ushindi huo, licha ya Ngoma kukosekana mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kufiwa na mdogo wake.

Hata hivyo, Yanga iliweza kuifunga timu hiyo jumla ya mabao 3-0, kwa kuwatumia vema Amissi Tambwe mshambuliaji raia wa Burundi na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.

Mafanikio hayo yanaifanya timu hiyo kuwa kwenye msimu mzuri, endapo kocha mkuu, Hans van der Pluijm, atazichanga vyema karata zake.

Kwani kocha huyo akifanikiwa anaweza kuwa wa kwanza kuweka rekodi kwa timu hiyo kuingia robo fainali kwani mara ya mwisho  kwa timu hiyo kufanya hivyo ilikuwa mwaka 1998.

Yanga iliendelea kuonesha ubora hata ilipokuwa  ugenini kuikabili APR hatua iliyofuata ya Klabu Bingwa Afrika na kufanikiwa kutoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1, yaliyofungwa na beki wa kulia, Juma Abdul na Kamusoko.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo kuwa salama kwenye mechi wa marudiano itakayochezwa Jumamosi hii ambapo sare au ushindi wa aina yoyote utawavusha hatua inayofuata na kuwasubiri mshindi katika mechi iliyowakutanisha vigogo wa Misri, Al Ahly dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola.

Ari ya kikosi cha Yanga inaonekana dhahiri kuwa tayari kuikabili timu yoyote kwenye michuano inayoshiriki, hivyo itakuwa kazi ya kocha katika kuboresha kikosi kutokana na makosa yanayojitokeza mchezoni.

Wawakilishi wengine Azam, wao walianzia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, ambapo wamefanikiwa kuibuka kidedea ugenini kwa kupata ushindi wa bao 3-0 dhidi ya wapinzani wao, Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho.

Azam walikamilisha karamu ya mabao hayo kupitia kwa Salum Abubakar, Shomari Kapombe na John Bocco, ambao walionekana kuwa mwiba mchungu kwa wapinzani.

Baada ya mchezo huo, Azam inatarajia  kurudiana na Bidvest Jumapili hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kocha wa Azam, Stewart Hall, huenda akaweka kumbukumbu ya kipekee kwenye klabu hiyo kwa kucheza fainali ya michuano hiyo.

Ukiangalia mafanikio kwa klabu zote, utaona kwamba zinatakiwa kuamua kupambana ili kurudisha heshima ya soka la Tanzania na kuondoka kwenye dhana ya kuitwa washiriki badala ya wapinzani wa kweli.

Msimu huu unaweza ukawa wa mafanikio na kujibu maswali mengi yaliyojaa shaka kwenye vichwa vya Watanzania  na kuwafanya waendelee kufurahi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles