30.4 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Yanga, Azam kuzirahisishia kazi ya Simba?

WINFRIDA MTOI- DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga na Azam, zinatarajia kushuka dimbani leo, katika viwanja tofauti, katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga itanarajia kuvaana na Ndanda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam itakuwa ugenini mkoani Mara kuikabili Biashara United, mchezo utapigwa dimba la Karume, mkoani Mara.

Michezo hiyo miwili inatazamwa kwa jicho la tofauti kwani timu hizo zikiangusha pointi tatu Simba itatwaa ubingwa wa msimu wa 2019/2020 kabla hata ya mchezo wake wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Simba inaongoza ikiwa na pointi 78, Azam katika nafasi ya pili na pointi 58, Yanga ikifuatia kwenye nafasi ya tatu na pointi 57, zote zikishuka dimbani mara 31.

Kihesabu, Azam ikishinda michezo  yake yote iliyosaliwa nayo itafikisha pointi 79, Yanga itafikisha 78, wakati Simba itafikisha pointi 81.

Kutokana na hesabu hizo, Yanga na Azam zikipoteza leo ni wazi hakuna wa kuizuia Simba kutangaza ubingwa kabla ya Jumapili.

Azam na Yanga zinazopigania nafasi ya pili, leo zitakuwa na kibarua kigumu cha kusaka pointi tatu kutokana na ubora wa timu wanazokutana nazo, hali hiyo ikitokana na ushindani uliopo kwa sasa kipindi hiki.

Ukiangalia Yanga, kikosi chake kimekuwa si cha uhakika wa kupata matokeo kutokana na kuwakosa nyota wake kadhaa,hilo liliodhirishwa kupitia mechi mbili zilizopita ambazo ilivuna sare mfululizo.

Wanajangwani hao wataendelea kuwakosa, Bernald Morrison, Lamine Moro wanaotumikia adhabu ya kufungiwa mechi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pia Papy Tshishimbi na Jaffar Mohammed ambao ni majeruhi.

Udhaifu katika safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji, umefanya Yanga kuwa laini.

Azam itaingia uwanjani ikiwa na uchu wa wa kuvuna pointi tatu, baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar, katika mchezo wake uliopita Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.

Yanga inakutana na Ndanda inayosaka pointi tatu ili kujinusuru kushuka daraja huku ikitoka kulazimisha suluhu dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Azam nayo inakutana na Biashara ambayo ina rekodi nzuri katika uwanja wake wa nyumbani, ikitoka kuichapa KMC mabao 4-0 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, alisema hatapenda kuona kile kilichofanya na wachezaji wake katika mechi iliyopita.

Eymael akizungumzia mazingira ya kikosi chake alisema hawakucheza katika kiwango bora walipoikabili Azam kwani hawakutumia nafasi walizotengeneza kufunga, lakini siku mbili za  mazoezi zimetosha kuwaongezea makali wachezaji wake.

“Natarajia kuona mchezo mchezo mzuri, bado tunapambana kupigania nafasi ya pili, wachezaji wangu nimewaambia makosa waliyofanya kwa Namungo, nina imani hayatajirudia,” alisema Eymael.

Naye Kocha Mkuu wa Ndanda, Meja Mstaafu Abdul Mingange, alisema watarajia mchezo mgumu kutokana na ubora wa wachezaji wa Yanga.

“Yanga ni timu kubwa, hautakuwa mchezo rahisi kwetu na tunachotakiwa ni ushindi ili kuondoka huku tulipo, tutajitahidi kwa uwezo wetu ndani ya dakika 90 tutajua tumevuna nini,” alisema Meja Mingange.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Biashara United, Francis Baraza, alisema atawakosa wachezaji  sita wa kikosi cha kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo majeruhi, lakini amejiandaa na wale waliopo.

“Nimewaambia wachezaji wangu tunatakiwa kushinda mchezo huu ili tusiambiwe tumebahatisha kwa KMC, pia adhamu inakuja kucheza kwa hadhari kubwa baada ya kupoteza,” alisema Baraza.

Michezo mingine itakayopigwa leo,  Ruvu Shooting itaikaribisha  Namungo dimba la Mabatini, Pwani, Mbeya City itachuana na JKT Tanzania Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Jijini Mwanza, Alliance itapimana ubavu na wageni Coastal Union, Uwanja wa Nyamagana, Mtibwa Sugar itakuwa mgeni wa Mwadui dimba la Mwadui Complex mkoani Shinyanga.

Singida United itaikaribisha Lipuli Uwanja wa Liti mkoani Singida, Kagera Suga itakuwa mwenyeji wa KMC  dimba la Kaitaba, Bukoba.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,854FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles