32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Yanayoendelea nchini ni zaidi ya nyufa alizoziona Baba wa Taifa

NyerereWIKI iliyopita kulikuwa na kongamano lililoandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere pamoja na lile lililoandaliwa na Kavazi la Mwalimu Nyerere.

Tangu Mwalimu Nyerere alipotutoka kumekuwa na hali ya uwazi fulani katika yale aliyokuwa anayasimamia na kuyaamini. Uwazi huu ni bayana kwani kila mara panapotokea jambo imebidi vyombo vya habari kuweka sauti ya Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa ameweka majibu ya karibu kila tukio.

Hotuba zake za kabla ya mwaka 1999 alipofariki zina majibu ya masuala mengi yanayotokea sasa na hakuna ambaye amevaa viatu vya Mwalimu Nyerere katika kusimamia hayo.

Katika makongamano hayo suala lililokuwa linazungumziwa na urithi aliotuachia Baba wa Taifa. Kuna moja ya hotuba zake iliyo maarufu sana ya nyufa. Alikuwa ameainisha nyufa kama tano hivi alizoona zinaonekana katika taifa na akamtaka Rais atakayeingia madarakani akabiliane na nyufa hizo.

Huu ulikuwa ni urithi uliotolewa kama mausia kwetu na viongozi wetu.  Jambo ambalo nimelitafakari sana ni jinsi gani  urithi unatakiwa kupokelewa. Mtu anapotangulia mbele za haki na akaacha urithi kwa warithi wake kinachotegemewa ni wale waliorithi kuutumia vizuri ule urithi kwa faida yao na kwa faida ya kizazi kijacho. Kwa kuwa mwenyewe aliyetoa urithi huo hayuko wanaoupokea hujitahidi wafanye kama mwenyewe ambavyo angefanya au waboreshe zaidi. Hili huwa halitokei mara zote, wapo wanaopata urithi badala ya kuutumia vyema huutapanya na kuuharibu na hali yao huenda ikawa mbaya kuliko alipokuwepo aliyeacha urithi.

Sisi watanzania tulikuwa na bahati sana kama Taifa kuwa na mtu kama Baba wa Taifa kwani alikuwa ana maono ya mbali na ndio maana aliamua kuacha uongozi wakati hakuna sheria au katiba iliyokuwa ikimtaka kufanya hivyo. Aliweza pia kuhakikisha anaondoa hiyo hali ya kiongozi kuwa madarakani mpaka achoke mwenyewe. Na alipotoka madarakani aliweza kuwa muangalizi wa jamii na kupata nafasi ya kutoa maoni yake kwa yale aliyoyaona hayaendi sawa kiasi hata cha kuandika vitabu. Swali kwetu tuliyoachiwa urithi je  tumeupokea na kuufanyia kazi?

Tukiangalia moja ya nyufa Mwalimu alizozungumzia ni suala la Muungano, hili aliliongea mwaka 1995. Tujihoji kuhusu hali ya Muungano sasa  je imeboreka kuliko ilivyokuwa mwaka1995? Kama imeboreka ni kwa kuwa tulifuatilia aliyoyasema Baba wa Taifa au ni kwa bahati tu? Kama haijawa bora ni nini sababu?  Kuna suala la udini, ukabila, ukanda je haya nayo yalionekana kuwa na nyufa na Baba wa Taifa akatutahadharisha je hali ikoje kwa sasa? Hebu tujikumbushe kidogo tu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Huu ni mwaka niliposikia watu wakisema kuwa haitawezekana Rais kutoka kaskazini, huu ni wakati tulishuhudia watu wakizungumza zamu za viongozi kwa udini wao, lakini pia masuala ya ukabila na ukanda yalipamba moto.

Pia tulishuhudia kampeni zikipigwa kwa kilugha. Mwalimu alikuwa amejitahidi sana kujenga utaifa na kila mtanzania alikuwa huru kuishi popote hapa nchini. Kwa hiyo ukiwa Singida pamoja na kuwa kuna watu wa makabila fulani huko bado wapo wengi ambao si wa makabila hayo. Na mtu angeweza kuchaguliwa ambaye wala asili yake si mkoa huo. Sasa ukimkuta mtu anaongea kilugha katika mkutano wa hadhara ambapo kuna watu wa makabila mengi unajiuliza tunakwenda mbele au tunarudi nyuma? Ile sauti ya Baba tumeisikia au tumepotezea?

Ufa mwingine ulioongelewa ni ule wa suala la katiba na sheria. Mwalimu alitahadharisha suala la kupuuza, kutoijali na kuchezea chezea katiba. Huu ufa aliouona Mwalimu mwaka 1995 wa viongozi kupuuza, kuchezea katiba na kutoijali kwa sasa hali ikoje?  Tulipokuwa tunajitafakarisha tukaiangalia hali tuliyo nayo kwa sasa kwenye eneo la katiba.

Bila kuangalia suala la mchakato wa katiba ambao umesimama kimya tena kimya kikuu, tunaangalia hata hii katiba iliyopo kwa sasa. Kwa kiasi gani inaheshimiwa na haipuuzwi au kuchezewa kama Mwalimu alivyoonya.

Nilipata kuangalia kifungu kimoja tu katika katiba yetu na kufanya uchambuzi kidogo sana. Ibara ya 3 ibara ndogo ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977 inasema kuwa ‘Jamhuri ya  Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa’.

Iwapo  tunaweza kusema ufa wa kupuuza katiba umefutwa inabidi tuangalie hii ibara ambayo inatuonyesha Jamhuri yetu ni nini. Je hii Jamhuri ni kweli ni nchi ya Kidemokrasia? Misingi mikuu ya demokrasia nikiitaja kwa uchache tuanze na msingi wa ushiriki wa wananchi, usawa, stahamala za kisiasa kwa uchache. Kwa kuwa demokrasia ni utawala wa watu  uliowekwa na watu kwa ajili ya hao watu, sisi raia wa Tanzania ndio hao tulioweka watawala kwa ajili yetu.

Tunajisikia kuwa ndio tuliowaweka na wapo kwa ajili yetu? Huo utawala uliopo ni wetu? Kila  mmoja ajibu kwa jinsi anavyojisikia kuwa sehemu ya utawala wa nchi hii. Nchi hii ni ya Kijamaa, ni nini kinachoashiria ujamaa katika nchi yetu hadi katiba kusema nchi ni ya kijamaa? Nilikuwa nakumbuka jinsi ambavyo nchi ilikuwa imejengwa katika hiyo misingi ya kijamaa moja wapo ikiwa ni utu na undugu. Hivi ni nini kilitokea  tukaacha kuitana ndugu na uheshimiwa ukaanza tena kwa kasi? Sikatai kabisa watu kuitwa waheshimiwa lakini najiuliza tu swali dogo.

Huu utawala wa watu unawaweka watu kuwa viongozi kwa niaba yao. Ajabu ni kuwa sisi ambao tunampa mtu kazi ya kutuongoza ghafla tunageuka na yule tuliyemtuma anakuwa mheshimiwa sisi tuliempa kazi tunakuwa wakumpigia saluti na tusipofanya hivyo huenda tukanyimwa mshahara.

Hii hali ya watu kuchinjana kwa kasi bila huruma inatokana na nini? Utu uko wapi? Tumeielewa vizuri hii katiba yetu? Ni kweli kuwa hatufahamu kuwa waliompa mtu kura ndio wakuu na si vinginevyo? Ujamaa ndio ulipoanza kuzimika.

Lakini katika ujamaa matabaka huwa hayapo na kama yapo si kwa kiasi cha kuonekana hadi kuleta shida. Sasa hivi matabaka yapo wazi. Walionacho wameongezeka na walichonacho kimeongezek. Wasionacho wameongezeka na wasionacho kimezidi kupungua, matabaka yamezaa chuki na wimbi la wizi, ujambazi na kadhalika.

Ndio maana sehemu nyingi hasa za mijini matabaka yalipo bayana zaidi imebidi watu wawe jela katika nyumba zao, machuma madirishani na milangoni kuta kubwa na nene nyingine zikiwa na nyaya za umeme juu au chupa kali kuzuia wezi. Mbwa wakali na walinzi ndio hali halisi.

Huenda si sababu lakini tathimini ndogo tu ya hali ilivyoanza kubadilika inatoa picha hii. Ukija kwenye suala la kuwa nchi hii ni ya mfumo wa vyama vingi,  hili nalo ni swali la kujiuliza. Ni kweli kabisa tangu mwaka 1992  katiba ndio ilibadilika na kifungu hiki kikawekwa na mfumo ukaanza.

Tangu tuanze mfumo huu kiasi gani tunaiheshimu katiba katika kukuza mfumo huu? Mbona walio katika upinzani kwa mujibu wa katiba wanaonekana kama vile ni wahalifu? Huwa nasikia watu wakisema ‘ hata ninyi ni chama cha upinzani’ kama vile kuwa chama cha upinzani ni ukoma? Iweje vyama hivi ndio kila mara viwe vinazuiwa kufanya mikutano yao ya nje na sasa hata ya ndani?

Kuna wakati Katibu Mkuu wa Chama tawala alizunguka karibu nchi nzima akifanya shughuli mbalimbali zikiwemo za kijamii na mikutano ya hadhara. Sikuwahi kuona  akizuiwa na polisi  hata mara moja. Lakini vyama hivi vya upinzani kuanzia vilipoanza ndio masuala ya  maji ya kuwasha, mabomu ya machozi yalivyokuwa dhahiri zaidi. Kuna mtu aliyeandika katika makala fulani kuwa Tanzania imewahi kuwa na uhaba wa vitu vingi kama vile sabuni, mafuta ya petroli na hata sasa sukari lakini haijawahi kuishiwa mabomu ya machozi pale inapobidi kuwakabili wapinzani. Sijui kama ni kweli lakini ndivyo alivyoona huyu ndugu.

Mambo yanayoendelea sasa nchini kuanzia hali ya Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kufutwa, hali ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ambapo baadhi ya wabunge wamezuiliwa vikao kwa sababu mbalimbali.

Upendeleo wa wazi unaoonekana huko bungeni. Mfano Mbunge wa chama Tawala aliyewanenea wabunge wanawake wa vyama vya upinzani maneno ya kashfa ambayo pia yalihitaji uthibitisho akiachiwa kuendelea na vikao bila kutakiwa kukanusha au kuomba radhi, wakati wengine wakiambiwa wamesema uongo na hivyo kuzuiliwa kuingia kwenye vikao. Hizi ni zaidi ya nyufa alizoziona Baba wa Taifa.

Mwalimu aliwahi kusema TUJISAHIHISHE. Hapa tulipofikia ni kama tumechezea urithi wetu toka kwa Baba yetu wa Taifa, tuna uwezo wa kurekebisha kama tunahitaji kusonga mbele. Utashi wa Kisiasa na kuurejesha mchakato wa Katiba mpya huenda vikatutoa hapa tulipo.

Mwandishi ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles