Na JANETH MUSHI-ARUSHA
NOVEMBA 24 mwaka huu kote nchini unatarajiwa kufanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,ambapo Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ndiyo yenye jukumu la kuratibu na kusimamia uchaguzi huo.
Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa hufanyika kila baada ya miaka mitano kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288.
Aidha, uchaguzi utakaofanyika mwaka huu utakuwa wa sita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania mwaka 1992.
Katika Uchaguzi huo, wananchi watapata fursa ya kuchagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mtaa, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na wajumbe wa kamati ya mitaa, ambapo kufanyika kwake kuwapa fursa wananchi waweze kuchagua viongozi watakaowawakilisha katika shughuli za kujiletea maendeleo.
Tamisemi imeandaa mwongozo, kanuni mbalimbali za kusimamia uchaguzi huu ukiwamo Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019.
Wizara hiyo itashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu hiyo, mwongozo unaoainisha baadhi ya wadau kuwa ni vyama vya siasa, asasi za kidini, kiraia, kijamii na zile zisizo za kiserikali, vyombo vya habari, taasisi za Serikali na Vyama vya watu wenye ulemavu.
Pamoja na mambo mengine, unazungumzia umuhimu wa elimu hiyo na malengo yake, wajibu wa wadau hao, utaratibu na usimamizi wa utoaji wa elimu ya mpiga kura na njia zinazotumika kutoa elimu.
Tayari wizara hiyo imeshatoa ratiba ya uchaguzi huo ikiwamo kutolewa tangazo la majimbo na mipaka Septemba 13, huku Septemba 16 hadi 22 kukitarajiwa kufanyika uteuzi wa wasimamizi wasaidizi na wasimamizi wa vituo huku kampeni zikitarajiwa kufanyika siku saba kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Huku uandikishaji na uandaaji wa orodha ya wapigakura ukianza siku ya 47 kabla ya siku ya uchaguzi, ambao utafanyika kwa muda wa siku saba kwa kutumia fomu zilizoanishwa katika Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019.
Wadau mbalimbali wameanza kujiandaa kutoa elimu juu ya uhamasishaji wa uchaguzi huu ikiwamo kuelimisha makundi mbalimbali kama vile wanahabari juu ya masuala ya uraia na kuripoti kwa usahihi masuala ya uchaguzi.
Mtandao wa Asasi za Kiraia wa kuangalia Chaguzi Tanzania (TACCEO), kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na TAMISEMI wameanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari yenye lengo la kuwaongezea uwezo katika kuandika habari zenye kutoa elimu ya uraia kwa umma pamoja na uchaguzi kwa kuandika habari zenye tija na kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Katika makala haya, nitazungumzia juu ya umuhimu wa elimu kwa mpiga kura, ambapo kwa tafsiri rahisi ni elimu ambayo hutolewa kwa wananchi kuhusu masuala ya uchaguzi yenye lengo la kuhamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki katika tukio hilo kwa kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na miongozo inayosimamia uchaguzi.
Kwa mujibu wa mwongozo huo wa elimu ya mpiga kura, unaoratibiwa na kusimamiwa na Tamisemi, lengo ni kuhamasisha na kuwawezesha wananchi na wadau wa uchaguzi kuelewa mchakato wote wa uchaguzi, kanuni na taratibu ili waweze kushiriki na kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa.
Elimu hiyo itawawezesha wananchi kutambua haki na wajibu wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kushiriki kikamilifu kuchagua viongozi wanaowataka. Mwongozo utakaowezesha wadau watakaoshiriki kutoa elimu kuwa na taarifa sahihi za uchaguzi huo na kuwajibika kutoa elimu kwa kuzingatia misingi iliyobainishwa katika kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa mwaka 2019.
Mwongozo huo unaainisha elimu ya mpiga kura itatolewa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo mikusanyiko rasmi ya watu, mikutano na wadau, vipindi vya redio na runinga, makala za magazeti, mitandao ya kijamii na machapisho ya vijitabu, vijarida, vipeperushi, mabango na mavazi yenye ujume kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Unabainisha kuwa elimu ya mpiga kura itatolewa kwa kuzingatia uwepo wa makundi maalum ambayo ni muhimu kupatiwa elimu hiyo, vifaa na njia zitakazotumika kutoa elimu hiuo vitazingatia uwepo wa makundi maalum ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika kutoa elimu hiyo.
Makundi maalum yametajwa kuwa ni watu waliojitenga kwa sababu za kijiografia na shughuli za kiuchumi, mfano wafugaji, wakulima, wawindaji ambapo katika kutoa elimi kwa umma kwa kundi hili ni muhimu kuzingatia misimu yao ya kilimo, hali ya hewa na kwa wafugaji ratiba zao za kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kundi lingine ni la watu wenye ulemavu, ambalo linajumuisha wasioona, wenye ulemavu wa kusikia, walemavu wa ngozi na wenye ulemavu wa viungo ambao wote kwa pamoja kunahitajika umakini zaidi katika kuwahudumia kwa kuzingatia aina ya ulemavu mfano kutumia lugha za alama na nukta nundu.
Unasema kuwa kundi la wasiojua kusoma na kuandika,ili kufikisha ujumbe katika kundi uili ni muhimu kutumia njia za picha na maelezo, huku kundi la wanawake likianishwa kuwa ni kundi maalum kutokana na kuwa na majukumu mengi ya kifamilia na mfumo dume.
Vijana wameainishwa kuwa ni kundi maalum kwa sababu uelewa wao kuhusu umuhimu wa uchaguzi ni mdogo, hivyo kunahitajika kutumia njia ambazo zitawavutia vijana wengi kushiriki katika Uchaguzi zikiwamo mitandao ya kijamii, matamasha ya muziki, ngoma za asili na mihadhara rasmi.
“Wazee, wanaainishwa kuwa ni kundi maalum kutokana na umri wao pamoja na uwezo wa kuelewa masuala mbalimbali kulingana na mabadiliko ya sasa hususani matumizi ya teknolojia, pia uhusiano na rika zingine hivyo, elimu ya kundi hili ni muhimu itolewe kwa kuzingatia mahitaji ili wazee pia wapate fursa sawa ya kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” inaongeza.
Mwongozo huo unatoa wajibu wa wadau kuwa ni pamoja na kila mdau atakayepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura anatakiwa kuheshimu na kuzingatia sheria za nchi, kutumia kwa usahihi mwongozo huo, kuzingatia masharti ya usajili, kuwa mzalendo, kuheshimu na kulinda maslahi ya nchi na utamaduni wa Mtanzania.
“Kutambua makundi maalum katika jamii wakati wa utoaji elimu, kuweka wazi taarifa za mapato matumizi ya fedha zitakazotumika na zilizotumika kutoa elimu ya mpiga kura, kuhakikisha anatoa elimu katika eneo na muda alioruhusiwa, kuomba ufafanuzi Tamisemi endapo kuna suala hajalielewa na kutoa fursa ya kuuliza na kujibu maswali kwa ufasaha,” unasema mwongozo.
Mambo ambayo hayapaswi kufanywa na watoa elimu ya mpiga kura yanatajwa ni pamoja na kutumia mwongozo mwingine wa kufundisha zaidi ya huo uliotolewa na Wizara hiyo,kuhusisha elimu ya mpiga kura na ushabiki wa kisiasa au itikadi za vyama vya siasa,kujihusisha na rushwa.
“Kutoa elimu inayolenga kuwagawa wananchi katika misingi ya dini, rangi, makabila, jinsia, maeneo na ulemavu na kukasimu kazi ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa taasisi nyingine ambayo haikupewa kibali cha kufanya kazi hiyo,” inasema.
Mbali na yaliyoanishwa katika mwongozo huo ni wazi kuwa elimu zaidi inapaswa kuongezwa hasa katika uandikishaji wa wapiga kura ambapo hata katika chaguzi mbalilmbali za marudio pamoja na Uchaguzi Mkuu kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kutokujiandikisha au wengine kujiandikisha na kutokujitokeza kupiga kura.
Jamii inapaswa kutambua umuhimu wa kushiriki mchakato wa uchaguzi kuanzia mwanzo hadi mwisho ikiwa ni pamoja na kujiandikisha na kupiga kura ili kupata viongozi wanaofaa na kuwa watakapodharau kupiga kura kwa viongozi wa ngazi za chini ndivyo watakavyokuwa na wawakilishi wasiofaa.
Katika mafunzo yaliyotolewa na Tacceo mjini Dodoma hivi karibuni, Mwandishi Mwandamizi hapa nchini ambaye pia ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo kwa wanahabari kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kati, Ndimara Tegambwage, anasisitiza wanahabari kuepuka kuandika habari za mvumo na badala yake kuandika masuala yanayosaidia jamii hasa katika kipindi cha uchaguzi.
“Andikeni habari kwa ushahidi usiandike kwa mvumo, andikeni masuala yanayosaidia jamii ikiwemo elimu kwa wote ili kuhamasisha wananchi wachague viongozi kwa sababu wasipopiga kura maana yake umemchagua usiyempenda, elimisheni jamii kwa kutumia kalamu zenu,” anasema.
Mpiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni mtu yeyote ambaye ni raia wa Tanzania aliyefikisha umri wa miaka 18 au zaidi, awe mkazi wa eneo la kitongoji au mtaa husika, hana ugonjwa wa akili uliothibitishwa na daktari anayetambulika na Serikali au Bodi ya Utabibu na awe amejiandikisha kupiga kura katika kitongoji au mtaa husika.
Hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaeleza kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo ni vema kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi kwani uchaguzi ni suala la hiari na la kidemokrasia.
Wadau kwa kushirikiana na Tamisemi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wanazingatia na kutoa elimu kwa kufuata mwongozo huo ili kufikisha ujumbe kwa jamii.