24.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

YALIYOTOKEA SHULE YA MOI NI SOMO KWA WATANZANIA

Na Baraka Ngofira

SIKU za nyuma ilikuwa rahisi sana kusikia wanafunzi wa shule fulani wamechoma shule au mabweni. Muda mwingine walipokuwa wakigoma tu kitu cha kwanza ambacho walikuwa wakikifanya ni uchomaji wa ofisi muhimu za shule ikiwemo stoo ya chakula, mabweni yao na hata ofisi za walimu.

Lakini kwa muda sasa matukio hayo yamekwisha na sasa hayasikiki tena na migomo mashuleni pia ni kama imekwisha kabisa. Itakumbukwa shule ambazo zilikuwa vinara wa migomo na uchomaji wa shule ni kama vile Mara sekondari, Ikizu, Njombe, Lupata, Tarime sekondari, Tosamaganga, Lyamungo, Umbwe, Old Moshi, Karatu na nyinginezo nyingi.

Katika matukio hayo yote ya migomo na uchomaji na uharibifu wa miundombinu ya shule kwa kiasi kikubwa hayakusababisha vifo vya wanafunzi au walimu katika shule hizo. Japo hayo yamepita na sasa hali ni shwari katika shule hizo, lakini kuna umuhimu mkubwa wa viongozi waliopo kuhakikisha kuwa hali hizo hazijirudii tena.

Katika siku za hivi karibuni Shule ya Sekondari Moi iliyopo nchini Kenya iliungua na kusababisha vifo vya wanafunzi 9, ambao waliteketezwa vibaya kwa moto na kushindwa kufahamika hadi kwa vipimo vya DNA.

Lakini pia wengi wao wakiwa wamejeruhiwa vibaya kwa kuunguzwa na moto. Tukio hili la ajabu na la kinyama kabisa kwa taarifa za awali linaonyesha kuwa lilifanywa na watoto wadogo tu tena mabinti wa takribani miaka 15 hivi. Ambao walichukua uamuzi huo baada ya kunyimwa ruhusa ya kwenda nyumbani kwa sababu walizozijua wao.

Ndipo wakachukua uamuzi huo wa kuteketeza shule na kusababisha madhira makubwa kiasi hicho. Nitumie fursa hii kuwapa pole Wakenya wote kwa tukio hili lakini kwa namna ya pekee wazazi na ndugu na jamaa wa wanafunzi waliopoteza maisha katika tukio hilo. Lakini pia wale waliojeruhiwa Mwenyezi Mungu awajalie ahueni ili waweze kupona haraka warejee katika masomo yao.

Kwa tukio hili lazima walimu na wamiliki wa shule wajitafakari waone je, miundombinu ya shule zao ni rafiki kwa wanafunzi hasa majanga ya moto yakitokea. Maana kuna baadhi ya shule hasa katika mabweni wanafunzi wanapolala wanalazimika kuzima taa na kufunga milango kwa kufuli kwa kuogopa wezi au wanafunzi kutoroka.

Jambo ambalo kwangu naliona ni mtazamo hasi kabisa, kwani kila ninapofikiria vifo vilivyotokea katika shule ya MOI roho yangu inajawa na ganzi na kubaki na kujiuliza hadi hao wanafunzi 9 wanateketea kwa moto kiasi cha kushindwa kufahamika, wenzao walikuwa wapi kuwaokoa. Huku nikiyafikiria hayo najiuliza tena kwanini kuna kiasi kikubwa cha wanafunzi katika bweni hilo walijeruhiwa?

Jibu la haraka haraka linalonijia akilini mwangu ni kuwa huenda bweni hilo lilikuwa limefungwa na hata njia mbadala za kujiokoa kama vile madirisha ya wazi au vioo ambayo ni rahisi kuvunjika na kuokoa maisha ya watu hayakuwepo. Badala yake madirisha yalikuwa ni ya nondo tena zile nzito zilizosokotwa kwa maua ndizo zilikuwepo katika bweni hilo.

Tuje kwenye shule zetu je, mabweni yake yana miundombinu gani? Je, madirisha yake ni ya namna gani? Na vitanda je? Lakini mbali na hayo je, ni shule ngapi ambazo katika mabweni ya wanafunzi wanalala huku mabweni yao yakiwa yamefungwa na funguo kulala nazo walezi wa wanafunzi hao au kiongozi wa bweni kwa kuhofia wezi na wanafunzi kutoroka?

Lakini ni shule ngapi ambazo kwa kuogopa gharama za umeme kuna ratiba kabisa za kuwasha na kuzima taa za mabwenini? Tukishajiuliza hayo yote tujitafakari je, yakitokea kama yaliyotokea Shule ya Sekondari Moi ni shule gani itapona?

Ukiachilia mbali hayo pia kuna baadhi ya shule kwa tamaa za fedha hasa za binafsi na mashirika ya dini hubeba wanafunzi kupita kiasi. Na kuwalazimu wanafunzi kulala zaidi ya mmoja na wengine kulala madarasani au chini katika korido za mabweni hayo. Hivi kweli tutapona au ndiyo tutasubiri uchunguzi usiokuwa na mwisho na hatimaye inabaki historia?

Mbali na Serikali kutaka kila shule au taasisi kuwa na vifaa vya kuzimia moto maarufu kama ‘fire extinguisher’, lakini kuna shule hazina kabisa hata moja. Na kama zipo basi zimetunzwa katika ofisi ya mkuu wa shule au ofisi za walimu au katika maabara kama ipo. Na shule nyingine zipo tu kama mapambo maana hakuna mwanafunzi hata mmoja anayejua namna ya kuitumia endapo janga la moto likitokea.

Ni rai yangu kwa Serikali na wadau wote wa elimu ikiwemo wamiliki wa shule kuhakikisha kuwa shule wanazozijenga zinakuwa na miundombinu rafiki ambayo majanga ya moto yatokeapo uokoaji unakuwa rahisi. Na hata kama yakitokea madhara basi yawe kidogo tu.

Kwa mfano Shule ya Sekondari Lyamungo iliyopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro mbali na majaribio uliokuwa ukifanywa na wanafunzi wa shule hiyo, lakini hawakufanikiwa hata siku moja zaidi ilikuwa wanachoma vitu vyao wenyewe na hivyo hasara ilikuwa kwa wahusika na si shule.

Pia ni lazima kwa shule zote nchini kuwa na ving’amuzi moto au fire alarm ili hata ikitoka itilafu ya umeme ambao unaweza kusababisha moto vile ving’ora vya tahadhari vitasaidia kuwaamsha hata wale walioko usingizini. Na kwa kufanya hivyo itasaidia kuokoa maisha ya wanafunzi katika shule zetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,451FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles