24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Yaliyomkuta Kitwanga kabla ya kung’olewa

Charles Kitwanga*Aliwekewa makachero wa kufuatilia nyendo zake, Dar, Dodoma na Morogoro

 

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimepita siku sita tangu Rais Dk. John Magufuli amng’oe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kwa ulevi, mengi yamezidi kuibuka hadharani.

Pamoja na uamuzi huo wa Rais Magufuli, imeelezwa kuwa Kitwanga pamoja na timu yake walikuwa wakifuatiliwa nyendo zao na makachero.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa moja ya taarifa ambazo ziliwasilishwa na makachero hao kwa Rais Magufuli ndizo zilisababisha kiongozi huyo kulazimika kuchukua hatua hiyo.

“Unajua Kitwanga alikuwa akishughulikiwa muda mrefu bila yeye mwenyewe kujua, na hata kuondolewa kwake hadi sasa haamini. Wapo waliodai kuwa baada ya kuwasilisha bajeti yake Mei 16, mwaka huu alikwenda kulala Morogoro badala ya nyumbani kwake mjini Dodoma katika eneo la Sengia (Site 11).

“Lakini pia inadaiwa kwamba  kwa muda amekuwa halali nyumbani kwake na badala yake kwenda katika moja ya hoteli (jina linahifadhiwa) mjini Dodoma ambako hulewa hadi asubuhi jambo ambalo si la kweli, ni kama mkakati wa kumshughulikia… na si hivyo tu, hata baadaye zilitolewa taarifa kuwa yupo Morogoro, ambako pia watu walimfuatilia kwa karibu, lakini kwa bahati nzuri hakuwepo.

“Tena si hilo tu, hata pia eti wanadai alilewa sana kwa kunywa Vodka hali ya kuwa hatumii kinywaji hicho, na bila kujijua tangu usiku alipokuwa na madiwani wake (Mei 19), alikuwa akifuatiliwa na vyombo vya dola, tena walikuwa wakitumika wanawake ambao kama ndio walikuwa wakiandaa taarifa mbaya dhidi yake,” alisema mtoa habari huyo ambaye yupo karibu na mbunge huyo wa Misungwi.

Chanzo hicho cha habari kilisema kuwa pamoja na hali hiyo, wapo baadhi ya vigogo kutoka katika mashirika na taasisi nyeti za Serikali ambao walikuwa na vita ya kufa na kupona dhidi ya Kitwanga, hadi kufikia kufanya vikao vya siri vya kumshughulikia.

Mtoa habari huyo alisema kuwa mipango hiyo ilipangwa kwa ustadi mkubwa, ambapo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo kuna baadhi ya watu walikuwa wakimfutilia kwa karibu wakiwemo ndani ya idara zilizokuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Unajua huyu bwana alianza kushughulikiwa muda kidogo tangu siku ilipotolewa taarifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, iliyoeleza kwamba naye hakujaza fomu ya maadili ya viongozi wa umma, yeye pamoja na mawaziri wenzake akiwemo Balozi Augustino Mahiga na January Makamba, ingawa nguvu kubwa ilikuwa kwake.

“Na tangu wakati huo haukupita muda kidogo likaibuka suala la Lugumi na kama unakumbuka hapo alikuwa na vita ndani ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Uhamiaji ambako kote huko kuna watu waliwajibishwa,” alisema mtoa habari huyo.

Alisema pamoja na hali hiyo, katika kile ambacho kilikuwa kikiwatesa baadhi ya watu ndani ya Serikali ni hatua ya ukaribu kati yake na Rais Magufuli ambao kuna wakati zilisambazwa video katika mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwa na kiongozi huyo wa nchi wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

“Katika video hiyo anaonekana Kitwanga akiwa na Rais Magufuli uwanja wa ndege ambapo alikuwa akimuhamasisha achukue fomu ya kuwania urais, jambo ambalo alitekeleza baadaye na kufanikiwa kupita katika mchujo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Katika kile kinachooneka vita ya kimkakati kati ya makundi mawili ndani ya CCM, hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kundi moja linaonekana kufanikiwa kupitia kuondolewa kwa Kitwanga katika nafasi ya uwaziri,” alisema.

Baada ya kufutwa kazi kwa Kitwanga ndani ya Serikali ya Rais Dk. Magufuli, Mei 23, mwaka huu, kundi la madiwani  pamoja na wakereketwa wa jimboni kwake, wakiwamo Baraka Kingamkono, Gaudency Tungaraza na Iddy Majumuisho kupitia Kampuni ya CZ Information & Media Consultant Ltd walitoa tamko kumtetea Kitwanga huku wakidai kuwa watu wa Teknolojia ya Mawasiliano (IT) waliichezea video kitaalamu ili kufanikisha lengo la kuonyesha kuwa mbunge wao alikuwa amelewa bungeni.

Katika tamko hilo, madiwani na makada hao walidai kuwa walikuwa mkoani Dodoma, kwa kile walichodai walikwenda kumtembelea mbunge wao bungeni na walizungumza mambo mengi kwa ajili ya jimbo na kuambatana naye kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge, walikoshuhudia anajibu swali vizuri kabla ya kutoka naye nje na kupiga picha.

Pamoja na hali hiyo waliliomba Bunge kumuomba radhi Kitwanga kwa kile walichodai kumdhalilisha mbele ya wapigakura wake wa Jimbo la Misungwi, familia yake pamoja na Watanzania wote waliokuwa wanaamini utendaji wake.

“Tunamuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali bungeni atoe uthibitisho wa kikemia unaotanabaisha wazi kama Kitwanga alikuwa katumia kilevi wakati akiwa bungeni maana hakuna kipimo chochote kilichofanyika kuthibitisha uvumi huu.

“Tunaliomba Bunge lifanye uchunguzi na kubaini wale wote waliosambaza ile video inayoonyesha Kitwanga akiwa anaongea na kuonekana amelewa wakati kiuhalisia hakulewa na alijibu maswali yote vizuri. Tunaliomba Bunge kuchunguza Idara ya Habari ya Bunge pamoja na studio ile ya Bunge ambao wamehusika na kuhariri ile picha ya video iliyokuwa inasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunahoji uhalali wa kumvua mtu madaraka kwa sababu ya ulevi bila uthibitisho wa daktari ambaye kisheria ndiye mwenye mamlaka hayo kugundua kilevi cha mtu,” alisema Mkurugenzi wa Kampuni ya CZ Information & Media Consultant, Cyprian Musiba  katika tamko hilo kwa niaba ya madiwani na wananchi wa jimbo hilo.

Alisema Waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo imepotoshwa, bali ulikuwa ni mkakati wa kumchafua na kuhakikisha anavuliwa wadhifa wake ili watu waovu waendelee kufanya maovu yao

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles