24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Yaliyojificha kwenye Muungano wetu

 MWANDISHI WETU

MIAKA 56 imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na Wazanzibar liweke historia ya kung’oa nanga baada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi Aprili 26,1964. Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).

Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na mahusiano ambayo yalishabihiana kama si kufanana kwa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni na kihistoria zilizochangia huu muungano wetu.

Kutokana na sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika kwamba Visiwa vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata kushikamana kwa pamoja pembezoni mwa Pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu awali tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.

Pia, kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya wakazi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi kushamiri baina yao.

Hali kadhalika harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia kutuunganisha. Inaaminika (na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.

Licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki katika mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar hata hivyo kulikuwepo na asilimia kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda yake yalionekana ya Mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na ghiliba za Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili, hatimaye waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.

Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake zilianza kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Aprili 22, 1964, maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Nyerere (wa Jamhuri ya Tanganyika) na Karume (wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ) walitia sahihi Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano” na hivyo kuunda 

 Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni muungano sahihi kabisa kisheria na unaotambulika Kikatiba.

Siku ya Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja tu la kubadilishana “Hati za Muungano”.

Waasisi wa Muungano, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kushoto) na Hayati Abeid Aman KarumeWananchi wa Tanzania walipiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza kabisa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.

Kama nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa kutiwa sahihi mkataba unaoitwa Hati ya Muungano (Articles of the Union) na wakuu wa nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964 na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizo Aprili 25, 1964 na hatimaye kuwa sheria ya Muungano ya (Acts of Union) ya mwaka 1964.

Kimsingi sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo iliyopewa haki ya chombo cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za Serikali ya Muungano.

Mwanzoni Hati ya Muungano (Articles of Union) iliyomo ndani ya sheria ya Muungano iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya Muungano. Mambo hayo ni kama vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama (lakini si usalama wa Taifa); Polisi, Uraia, Uhamiaji, Mikopo na biashara za nchi za nje, Utumishi katika serikali ya Muungano, Kodi ya mapato, Usimamizi wa fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.

Kwa nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele kwa malengo kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule tulioanza nao awali na hali kadhalika maridhiano yanayoendelea kuufanya Muungano huu uendelee kudumu hadi hii kesho.

Ndio maana mtu timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea kuboreshwa kila siku (na itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11 ambapo hii leo yamefikia takribani 23.

Mengineyo ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama vile;- Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa za mafuta na gesi asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti; utabiri wa hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979; pamoja na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa.

Tusisahau mwaka 1965 iliundwa Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of The United Republic of Tanzania) mpaka kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.

Mwaka huo huo (yaani miaka 13 baada ya Muungano kutokea) kulikuwa na muungano wa vyama vikubwa viwili kuungana kutoka pande zote mbili (Bara na Visiwani). Vyama hivyo ni TANU (Tanganyika African National Union) pamoja na ASP (Afro Shiraz Party) cha Zanzibar kuungana na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) .

Hatua ama vitendo na mafanikio hayo si tu kwamba yalidumisha bali hata yaliendeleza kukuza Muungano wetu ambao Jahazi lake liligubikwa na misukosuko ya mawimbi makubwa baharini uliojaa uzito wa mambo mbalimbali uliokuja kwa sera ya kero zilizoleta chokochoko mbalimbali katika Muungano wetu., ambao hatutakiwi kamwe kuusahau maishani mwetu.

Tusisahau mchezo mchafu uliojaa rafu za kutisha uliotaka kufanywa na Bunge miaka ya 1990 na 1992 ya kutaka kuyakubali madai yaliyotolewa na kundi la G55 ambalo lilitaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika, hali hii ingetuvuruga kwani ilihitaji uwepo na serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika yatupasa tuzishukuru hekima na busara za Mwalimu Nyerere kwa kutuokoa na chokochoko ya kero hii.

Pia tusiisahau kero ama chokochoko nyingine ya Muungano wetu iliyoibuka Desemba 1, 1992, ambayo Zanzibar ilitaka kujiunga na umoja wa Nchi za Kiislam Duniani (OIC) kama nchi nje ya Muungano.

Tuendelee kukumbuka ni kwa jinsi 

 gani Zanzibar iliyokuwa inasaka ukuu nje ya Muungano kwa kuibua madai ya Bendera ya Taifa lake (Zanzibar), wimbo wa Taifa, na nembo yao ya Taifa.

Kwa nyakati tofauti tofauti huko nyuma tulisikia baadhi ya Wazanzibari walio wachache wakiilalamikia hali nzima ya ongezeko la mambo kwenye Hati Muungano (Articles of Union) kutoka mambo 11 hadi kufikia 23 ambalo ni sawa na ongezeko la mambo 12 ambao kwa baadhi yao hawaoni umuhimu wa uwepo wake na hata kutishia kujitoa. Ila asilimia kubwa ya Wazanzibari wanayaunga mkono, hali iliyo sababisha hoja ya wachache kuzidiwa nguvu.

Tulisikia huko nyuma jinsi gani Wazanzibari wanavyotaka jambo la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na aina nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia iondolewe katika masuala ya Muungano ili Zanzibar ipate kunufaika zaidi na maliasili zake.

Pamoja na hayo na kero nyingine ambazo ninaamini serikali na mamlaka husika zimekuwa zikifanyia kazi hata kama si sasa undugu na mwingiliano uliopo utalazimisha hayo yafanyike kwa sababu Muungano huu wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles