CALIFORNIA, MAREKANI
KAMPUNI ya teknolojia ya Yahoo ilidukua mamilioni ya barua pepe za wateja wake kufuatia ombi kutoka kwa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Shirika la Usalama wa Taifa (NSA).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Yahoo ilifanya udukuzi huo mwaka jana baada ya kutakiwa kufanya hivyo na taasisi hizo za usalama Marekani.
Kampuni hiyo ya teknolojia iliunda programu maalumu kukidhia matakwa ya asasi hizo.
Yahoo haijakanusha ripoti hiyo iliyofichuliwa juzi na katika taarifa yake rasmi, yahoo inasema ni kampuni inayozingatia sheria za Marekani.
Tukio hilo ni mlolongo wa kashfa ambazo Marekani imekuwa ikihusishwa kudukua taarifa za watu mbalimbali kuanzia raia wake, raia wa kigeni hadi viongozi wakubwa duniani.
Reuters haikuweza kubaini aina ya data ambazo Yahoo ilikabidhi kwa taasisi hizo na iwapo maofi sa wa usalama waliwasilisha kwa kampuni nyingine za mawasiliano ombi kama hilo.
Kwa mujibu ya wafanyakazi wa zamani, uamuzi wa Mtendaji Mkuu wa Yahoo, Marissa Mayer kutii amri hiyo kwa kutoa maagizo kwa watenda waandamizi ilisababisha ondoko la Afi sa Usalama wa Habari Mkuu, Alex Stamos Juni 2015, ambaye kwa sasa anashikilia wadhifa wa juu wa usalama katika kampuni ya Facebook Inc.