Na Samwel Mwanga, Uyui
SHIRIKA la World Vision Tanzania kupitia wafadhili kutoka nchini Japan limetumia zaidi ya Sh milioni 152.9 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kuinua Ustawi wa Mtoto katika jamii hususan latika nyanja ya elimu, afya na lishe, maji, usafi wa mazingira kupitia mradi wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Lutende AP katika wilaya ya Uyui mkoani wa Tabora.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Lutende AP, Ngasa Michael wakati akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka wa fedha 2021/2022 mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Kisare Makori katika hafla ya kutimiza mwaka mmoja wa utekelezaji wa shughuli zake katika Kata ya Lutende iliyofanyika katika kijiji cha Mwisole wilayani humo.
Amesema kuwa mradi huo ambao ni wa miaka 12 katika eneo hilo lenye vijiji vya Lutende, Mwisole, Itaga na Simbodamalu umepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu ulipoanzishwa Oktoba 1, 2021 kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Serikali na wananchi wa eneo hilo.
Amesema kuwa kwa kutambua majukumu yao katika jamii hiyo katika kutimiza kipindi hicho cha mwaka mmoja tangu waanze kutekeleza mradi huo wameweza kutengeneza madawati 590 kwa shule za msingi, kuwezesha upatikaji wa sare 600 za wanafunzi, madaftari 3,200, kalamu za wino 2,500 na penseli 730 kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Mratibu huyo amesema pia katika kuboresha Afya za watoto 500 kwa kuwakatia Bima za Afya iliyoboreshwa, kutoa vyeti vya kuzaliwa 208 kwa watoto waliozidi miaka mitano hasa wale waliotambuliwa kuwa na magonjwa sugu kama vile Selimundu ambao watapata fursa ya matibabu katika Hospitali za Rufaa kupitia uwezeshi wa shirika hilo sambamba na kutoa mafunzo ya lishe bora kwa watoto.
Amesema ili kuhakikisha masuala ya lishe yanazingatiwa katika jamii, wamegawa mbegu bora za viazi lishe vipando 50,000 vinavyotosha kupandwa ekari 4 kwenye kikundi cha Mafanikio kilichoko kwenye kijiji cha Lutende lengo ni kuboresha lishe katika kaya.
Amesema ili kukuza michezo na kupunguza utoro na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni wamewezesha jezi za michezo seti 10 na mipira 10 ambapo kila shule ya msingi katika kata hiyo itapata mipira miwili na seti mbili za jezi kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu na mikono.
“Tunayafanya haya yote kutokana na jamii kutupokea na kukubali kufanya kazi nasi na kwa kipindi cha mwaka mmoja tu tumeweza kufanya mambo haya makubwa katika jamii yetu ya Lutende, hivyo endeleeni kutupa ushirikiano mkubwa tuna imani hadi miaka 12 ya mradi wetu itakapokamilika kutakuwa na mabadiliko makubwa ya maendeleo kwenye eneo hili,”amesema.
Naye Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega, Jackline Kahihura amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zenye lengo la kuibadilisha jamii hasa katika kuboresha afya ya mtoto na mazingira ya kusoma na kujifunza katika shule za msingi katika eneo hilo.
Amesema wamebaini ya kuwa eneo hilo hasa kijiji cha Mwisole kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hivyo katika kipindi hiki cha utekelezaji wa mpango huo moja ya kazi waliyopanga ni kuchimba kisima kirefu cha maji kitakachogharimu kiasi cha Sh 130 ili wananchi wa kijiji hicho waweze kupata maji safi na salama.
“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali sisi pamoja na wafadhili wetu wa Japan kuwa ni sehemu ya kuchochea maendelo kwa wananchi wetu hapa nchini natumaini kwa miaka 12 tutakayokuwepo kwenye eneo hili la Lutende nikuhaidi mkuu wa wilaya tutafanya kazi kwa weledi mkubwa ili tuweze kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta zote ambazo tutazigusa, hivyo wananchi waendelee kutupatia ushirikiano,” amssema.
Mkuu wa wilaya ya Uyui, Kisare Makori ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo kabla ya kukabidhi vitu hivyo vilivyotolewa na shirika hilo kwa watoto, wanafunzi na shule amesema kuwa licha ya serikali kufanya kazi kubwa katika sekta ya elimu na afya lakini bado haijatosheleza hivyo kuwepo kwa wadau wengine wa maendeleo kama vile shirika hilo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii yetu.
Amesema kwasasa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imeweza kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita hivyo ameitaka jamii kulinda miundombinu ya shule inayoletwa na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kama vile shirika la World Vission ili iweze kusaidia watoto wetu hapo baadaye.
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia inafanya kazi kubwa sana katika nyanja zote ikiwemo ya elimu tumeshuhudia sasa elimu ya msingi hadi kudato cha sita kwa sasa inatolewa bila malipo na miundo mbinu inajengwa hivyo niwaombe wananchi tunzeni hii miundombinu iliyojengwa na serikali na ile iliyoletwa na wadau wetu wa maendeleo wakiwemo World Vision,”amesema.