Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Viongozi wa Wizara nchini zimepewa rai kufuatilia na kusimamia kwa karibu maafisa viungo ambao wanahusika kuweka taarifa kwenye mfumo ili Viongozi wawe na umiliki (ownership) wa taarifa zilizo katika mfumo huo.
Hayo yamesemwa leo Agosti 11, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene katika kikao kazi cha Mawaziri kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage Hazina jijini Dodoma.
“Kwa upande wa uwasilishaji wa Taarifa ya Ilani ya Chama Tawala, uchambuzi umeonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2022 ni Wizara 14 pekee zilizowasilisha Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Ilani kwa mwaka 2022 na Wizara 13 hazijawasilisha.
“Taarifa za Mpango kazi hutakiwa kuwasilishwa kwenye Mfumo wa ‘DASHBOARD’ mwezi Januari kila mwaka. Aidha, kwa upande wa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha nusu mwaka, ambazo hutakiwa kuwasilishwa Julai 2022 ni wizara 4 zilizowasilisha,” amesema Simbachawene.
Amesema kwa mwaka 2022 wamepokea maelekezo yako kuwa Taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 itawasilishwa mwezi Novemba, 2022.
“Ili kuratibu taarifa hiyo vyema na kwa wakati, napenda Mawaziri kuratibu taarifa katika maeneo yanayowahusu na kuhakikisha zinawasilishwa kwa wakati kupitia mfumo huo,” amesema Simbachawene.