30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yaomba Sh trilioni 4, yakiri kukabiliwa changamoto ya corona

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WIZARA ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasilino imewasilisha bajeti yake ya zaidi ya Sh trilioni 4 huku ikikiri kukabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa corona.

Imesema hali hiyo imeleta hofu kubwa katika sekta ya uchukuzi, hususan kwenye bandari na viwanja vya ndege, hivyo kuathiri utendaji wa taasisi zinazotoa huduma katika maeneo hayo.

Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Isack Kamwelwe aliliomba Bunge limuidhinishie bajeti ya zaidi ya Sh trilioni 4.784.

Kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.616 ni kwa sekta ya ujenzi na zaidi ya Sh trilioni  3.152 sekta ya uchukuzi huku Sh bilioni  15.654 ni kwa sekta ya mawasiliano.

Waziri Kamwelwe alisema katika utekelezaji wa majukumu yake, wizara ilikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ugonjwa wa corona.

“Hali hii imeleta hofu kubwa katika sekta ya uchukuzi, hususan kwenye bandari na viwanja vya ndege, hivyo kuathiri utendaji wa taasisi zinazotoa huduma katika maeneo hayo. 

“Wizara inaendelea kuchukua tahadhari katika vituo vya mipakani, viwanja vya ndege na maeneo ya bandari ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona,” alisema Kamwelwe.

Alisema pamoja na hali hiyo, vifaa vya kinga vimeendelea kutolewa kwa wafanyakazi katika maeneo hayo pamoja na utoaji wa elimu kwenye vyombo vya usafiri.

Kamwelwe alisema kuwa changamoto nyingine ni pamoja na mahitaji makubwa ya fedha kwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu na utoaji wa huduma za uchukuzi.

“Ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali inaendelea kujadiliana na wawekezaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za fedha ili kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Kamwelwe.

Aliitaja changamoto nyingine ni uvamizi, uharibifu na hujuma kwa miundombinu ya reli, hususan reli zenyewe, mataruma, vifungio na madaraja ambapo pia wizara inaendelea kushirikiana na vyombo vya dola ili kuwabaini wahusika wa matukio hayo ikiwamo kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Kamwelwe alisema Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetenga Sh bilioni 36.528 kutoka katika vyanzo vyake ili kusimamia huduma za usafiri ardhini.

Alisema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya kuimarisha ushindani na kuhakikisha kuwa huduma za usafiri wa ardhini zinakuwa endelevu, kuimarisha usalama, ulinzi na ubora wa huduma za usafiri wa ardhini.

Kamwelwe alisema katika mwaka wa fedha 2020/21, Bodi ya Usajili ya Majengo imepanga kusajili wataalamu 120, katika fani za ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi na fani zinazoshabihiana nazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles