21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Wizara ya Maliasili, Jeshi waungana kukabili uharibifu wa mazingira

Mwandishi Wetu, Katavi

Wizara ya Maliasili na Utalii imebadili mfumo wake wa usimamizi wa maliasili toka ule wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi (Paramilitary), ambapo kwa kuanza imetoa mafunzo ya kijeshi kwa askari 140 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kambi ya mafunzo ya kijeshi Mlele mkoani Katavi .

Mafunzo hayo yamehitimishwa leo Aprili 12 kwa sherehe ya kuwatunukia vyeti askari waliofuzu ambapo zoezi lilifanywa na mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu na katika hotuba yake amewataka askari hao kuhakikisha wanarejesha katika uoto wake wa asili maeneo yote ya misitu ambayo yameharibiwa.

Amesema ni matarajio ya serilikali baada ya askari hao kuhitimu pamoja na kazi yao ya msingi ya ulizi watafanya kazi ya kuhakikisha wanarejesha uoto wa asili uliopotea.

“Leo  mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli wa TFS lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mazingira, na hatuwezi kusema zisiendelee, zinatakiwa kuendelea katika namna ambayo haitaifanya nchi yetu kuwa jangwa.

“Kuhitimu kwenu hakumaanisha mnakwenda kuzuia maendeleo, kunamaanisha mnakwenda kushirikiana na wanaotaka maendeleo kwa kufanya kazi wakifikiria maendeleo endelevu,” amesema.

Kanyasu amesema hivi sasa nchi inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti, ukame, mvua nyingi na mafuriko ambapo vyote hivyo husababishwa na matumizi mabaya ya kazi za kiuchumi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu TFS, Profesa Dos Santos Silayo katika hotuba yake amesema taifa limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali za kiuhifadhi ikiwemo shughuli za kibinadamu pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa watumishi na mambo yote hayo yanapelekea mafunzo hayo kuwa muhimu katika uhifadhi wa mapori na misitu ya hifadhi nchini.

Amesema TFS imekuwa mstari wa mbele kwenda na mabadiliko hayo kwa kuanza kutekeleza mafunzo ya watumishi katika ngazi mbalimbali wakati ikisubiri mabadiliko ya muundo wa utumishi utakaotambua mabadiliko ya vyeo na majukumu ya kila siku.

“Pamoja na mafunzo hayo yanayofanyika tunaimarisha vikosi vya kufuatilia taarifa ambapo tuna kitengo cha intelejensia ambacho tunakiimarisha ili kiweze kutoa taarifa sahihi kwa askari wa misitu na kuchukua hatua bila kupoteza wakati,”amesema.

Aidha zoezi hilo limehudhuriwa na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira pamoja na wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,719FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles