20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

WIZARA YA ARDHI NI MFANO WA KUIGWA KUTATUA KERO ZA WANANCHI


MOJA ya kero kubwa ambayo imeumiza Watanzania kwa kipindi kirefu, ni suala la uwapo wa migogoro ya ardhi, ambayo kwa namna moja au nyingine, ilisababisha watu kupoteza uhai.

Haikuacha watu salama. Wapo Watanzania wengi walipoteza maisha na wengine kupata vilema vya kudumu maishani mwao, jambo ambalo linaumiza.

Migogoro hii ilifikia hatua mbaya kwa sababu baadhi ya kauli za viongozi waliopewa dhamana ya kuisimamia walikuwa wakitoa matamko tu bila kuchukua hatua stahiki ambazo zingeweza kupunguza tatizo hili.

Si nia yetu kueleza mambo mengi, lakini tumelazimika kusema haya kutokana na utendaji kazi mzuri unaofanywa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi tangu amekabidhiwa wizara hii.

Pamoja na naibu wake, Angelina Mabula, viongozi hawa wameonyesha kudhamiria kupunguza au kumaliza migogoro ambayo ilifika wakati matajiri walikuwa ndio wenye sauti.

Tulishuhudia watu wengi wenye kipato cha chini wakilia kudhulimiwa ardhi kwa jeuri ya fedha.

Moja ya kazi kubwa ambayo imefanyika ndani ya wizara hii, ni kupambana na watumishi wa Serikali ambao kwa jina maarufu wanaitwa ‘vishoka’, waliokuwa na mtandao mkubwa wa kushirikiana na matajiri kupora ardhi za wanyonge.

Pili, kuvunja mtandao mkubwa wa watumishi ambao walikuwa wanajiona ni miungu watu kwa kuuza viwanja zaidi ya kimoja kwa watu wawili, jambo ambalo kila kukicha lilizua migogoro.

Tatu, kazi kubwa ya kupambana na maofisa ambao walikuwa ni wapenda rushwa wakubwa na kikwazo cha kuwapatia haki wananchi waliokuwa wakipeleka madai yao.

Nne, uamuzi wa kurekebisha baadhi ya vitengo na kuwaondoa watumishi wasiokuwa waaminifu kumechangia kuleta mapinduzi ndani ya wizara hii ambayo kimsingi imepewa dhamana kubwa ya kusimamia ardhi.

Utendaji kazi huu, ndiyo umesaidia  kupungua kwa kasi mapigano ya wakulima na wafugaji katika mikoa ya Morogoro, Manyara na kwingineko ambako watu wengi walipoteza maisha.

Tunafurahi kuona hivi sasa kasi ya upimaji na utoaji wa hati miliki za ardhi unaendelea kwa kasi ya aina yake, jambo ambalo linapaswa kupongezwa kwa nguvu zote.

Juzi Waziri Lukuvi alitoa wito kwa Watanzania kwenda wizarani kwake Dar es Salaam kuchukua hati zao 5,000 ambazo zimekamilika kwa asilimia mia moja.

Kati ya hati hizo, zipo ambazo ni za kuuziana viwanja na nyingine kwa ajili ya mikopo ya biashara.

Hii ni hatua kubwa na nzuri inayoonyesha uchapakazi wa wizara hii.

Kutokana na kazi zinazofanywa na wizara hii katika kutatua migogoro inayowakabili wananchi, sisi MTANZANIA tunawasihi mawaziri na viongozi wengine kuiga mfano huu wakati wanapohudumu katika maeneo yao.

Pamoja na hayo, bado Waziri Lukuvi na timu wanapaswa kuendelea kuchukua hatua kali kwa halmashauri, manispaa na mamlaka za miji maana huko nako kunatokota kwa wingi wa kesi za migogoro ya ardhi.

Tunaamini kufanya hivyo, kutasaidia kurudisha nidhamu kwenye sekta ya ardhi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,097FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles