Bahati Mollel, TAA
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imefunga mashine 11 kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ili kukabiliana na wagonjwa watakaobainika kuwa na virusi vya homa ya corona, vilivyoanzia nchini China.
Katika mashine hizo, tano zinatumia kompyuta zinazopima joto la mwili la abiria bila kujitambua na mashine sita za mkononi ambazo abiria anapimwa endapo ataonekana kuwa na joto kali zaidi.
Kitengo Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza JNIA, kimesema kimejipanga kukabiliana na virusi hivyo.
Mdhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa JNIA, Dk. George Ndaki amesema mashine moja imefungwa kwenye jengo la watu mashuhuri (VIP), nyingine imefungwa Jengo la pili la abiria na tatu zipo jengo la tatu la abiria wakati za mkono zimegawanywa kwenye majengo hayo.
“Wataalamu wa afya wanaokuwa kwenye mashine zinazotumia kompyuta wanamtambua abiria mwenye joto kali mara anapopita mbele ya kamera na endapo litabainika ni zaidi ya nyuzi joto 37.4 anahakikiwa zaidi kwa kutumia mashine ya mkono huku akihojiwa zaidi juu ya afya yake na nchi aliyotoka ili kubaini endapo ana virusi hivyo.
“Hadi sasa hakuna abiria aliyebainika kuwa na ugonjwa huu, lakini tunaendelea kwanihapa Kiwanja cha ndege ni moja ya njia kuu au lango kuu la abiria hususan wa nje ya nchi wanapotumia kuingia nchini, na ndio maana tunawakagua na tunashukuru Serikali yetu kupitia Wizara ya Afya kwa kuwa na mashine hizi ambazo zinafanya kazi mara mbili na kwa uhakika zaidi ili kubaini abiria mwenye virusi, ambaye atapelekwa eneo maalum kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema Dk. Ndaki.