28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WINNIE MANDELA: MAMA WA TAIFA ANAYEACHA VUMBI LA USHUJAA AU UASI?


NA MWANDISHI WETU    |

KIFO cha Winnie Madikizela-Mandela, mke wa zamani wa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ambaye pia alipigana vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, kimezua mjadala nchini mwake namna ambavyo mwanaharakati huyo anastahili kukumbukwa. Upande wa viongozi wa jadi pamoja na wafuasi wake, wanataka Winnie akumbukwe kama mwanamke asiyekuwa na hatia nchini humo.

Huku wengine hasa wale ambao bado wapo katika mapambano ya awali wakiwa chini ya mwavuli wa watu weupe wanataka Winnie Mandela kukumbukwa kama mtu mbaya sana na aliyetenda uasi.

Lakini kwa mtu yeyote ambaye anataka kumwelewa vizuri Winnie Mandela, anapaswa kurejea historia na kuona namna ambavyo alinyanyaswa, kuaibishwa na kuteseka wakati wa mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Makala haya yanaelezea mambo muhimu yanayoendelea kwa sasa nchini Afrika Kusini ambayo ni kiashiria cha wazi cha kupata majibu kwamba iwapo Winnie Mandela alikuwa shujaa na muasi.

Kupigania uhuru

Winnie alikuwa mpigania uhuru, aliyeleta mapinduzi kwa kuwa mpambanaji wa ubaguzi wa rangi, hakuwa mwanaharakati wa kushika silaha na kutegemea mashabiki wa mitandaoni.

Mume wake wa zamani, Nelson Mandela, alimwachia watoto wadogo wawili wa kike kuwalea wakati alipofungwa gerezani mwaka 1962.

Winnie kuitwa mwanaharakati ni haki yake, kwa kuwa ni mwanamke aliyewahi kukakamatwa na kuwekwa gerezani akiwa na nguo zake za kulalia tu, huku polisi wakiwazuia ndugu zake kwenda kumwona na kuzuiwa kuwaona watoto wake.

Siku 491 ndani ya chumba cha mateso

Mwaka 1969, Winnie alifungwa gerezani kwa muda wa siku 491 na hakupata msaada hata wa pedi wakati alipokuwa katika siku zake kama ilivyo kawaida ya wanawake.

Gereza lake halikuwa la kawaida, ila maalumu kwa ajili ya kumtesa. Mateso aliyoyapata gerezani yaliandikwa katika kitabu kiitwacho “491 Days”, kinachoelezea kelele ya mwanamke aliyekuwa anapigwa na kuteswa gerezani kila kukicha.

Lakini Winnie hakukosa kupaza sauti ya kuwatetea watu weusi waliokuwa wakipambana dhidi ya ubaguzi wa rangi ulioendeshwa na wazungu wachache nchini humo.

Baadaye wakati ambapo viongozi wengi walipokuwa wanafungwa jela, Winnie alikuwa mstari wa mbele katika kuongoza harakati hizo akiwa pamoja na hayati Nelson Mandela.

Kiufupi ni kwamba, Winnie aliamua kuongoza mapigano ya kutetea watu weusi bila kuchoka wala kujali matatizo aliyokuwa akikabiliana nayo katika juhudi hizo. Alipobainika kuwa ana ushawishi mkubwa, Winnie alihamishwa katika makazi yake yaliyokuwa katika mji wa biashara wa Johannesburg, kwenda kukaa katika mji mdogo wa Brandfort ambayo ilikuwa ngome imara ya watu weupe.

Mji wa Brandford upo Jimbo la Orange Free ambapo katika miaka ya 1970 baada ya operesheni mojawapo za kupambana na ubaguzi wa rangi zilizokuja kujulikana zaidi kama “The Soweto Uprising”.

Lengo lao kubwa lilikuwa kumdhibiti pamoja na kupunguza nguvu zake kwenye harakati za kutetea watu weusi.

Hakuruhusiwa kupokea wageni ingawa alikuwa anaweza kusafiri kila siku kwenda posta kupiga simu, ili kuuambia ulimwengu juu ya mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Tangu kifo chake kitokee Aprili 2, mwaka huu, kile kilichoandikwa na watu wengi katika mitandao ya kijamii, kinaonesha wazi kuwa kuna baadhi ya watu hawafahamu historia ya Winnie Mandela.

Kuna wengine wamezungumzia juu ya urembo wake na wengine jitihada zake katika kutetea nchi yake. Tukubaliane kuwa Winnie pia hakuwa mkamilifu, alikuwa na makosa yake pia. Aliwahi kuhukumiwa kwa kosa la udanganyifu na alikamatwa kwa kosa la utekaji nyara.

Licha ya misukosuko hiyo, Winnie, alibaki kuwa mtu muhimu sana katika siasa za Afrika Kusini na kuwa mwakilishi muhimu wa wanawake waliopambana kufa kupona dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwa unaendelezwa na wazungu walio wachache nchini humo.

Katika siku za baada ya uhuru wa Afrika Kusini anakumbukwa zaidi kwa kuwa miongoni mwa wachache katika uongozi wa ANC waliomuunga mkono aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, katika kushutumu na kulaani vikali vitendo vya kuwashambulia wahamiaji wa Kiafrika huko nchini Afrika Kusini, ambayo yalibadikwa jina ‘Xenophobic’.

Pia amekuwa muungaji mkono mkubwa wa kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema, kilichojiengua kutoka ANC ambacho kilimkosoa vikali rais aliyeng’atuka Jacob Zuma.

Historia ya Winnie hadi kifo chake inabaki akikumbukwa zaidi kama mama wa Taifa la Afrika Kusini aliyesimama kidete dhidi ya ubaguzi wa rangi katika umri wake wote.

Licha ya kuibuka kundi la watu ambalo linadai kuwa Winnie hakupaswa kupewa heshima yoyote bado ukweli umedhihirika wenyewe kuwa mwanamama huyo anazidi kung’ara kama alivyokuwa enzi zake ingawaje amefariki dunia.

Kuzungushwa nchi nzima

Rais wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa na kiongozi wa chama tawala cha African National Congress (ANC), pia alipigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Ramaphosa, amekaribisha ushujaa wa Winnie Madikizela-Mandela katika harakati zake dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Rais Ramaphosa alisema, Afrika Kusini inaomboleza kifo chake na Serikali itashirikiana na familia wakati wa mazishi yake rasmi Aprili 14 mwaka huu.

“Kutakuwa na shughuli kubwa ya kuzunguka sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kumuaga Winnie, itakuwa kila jimbo. Tunapenda kutoa heshima na shukrani zetu kutoka kila kona ya nchi hii na duniani kwa ujumla,” alisema Ramaphosa.

Ramaphosa alikutana mara ya mwisho na Winnie mnamo Machi 10, wakati wa kuandikisha wapigakura.

“Mimi kama rais wa ANC, nimehuzunishwa kwa sababu nilikwenda kuhakikisha taarifa kwenye daftari la wapigakura nikiwa naye. Nilikula naye chakula.

Wafuasi wa Winnie mjini Soweto walikusanyika, wakiimba nyimbo za vita walizokuwa wakiimba wakati wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Mazishi ya Kijeshi

Pamoja na mjadala huo kukolea kwamba Winnie ni shujaa au la, Serikali ya Afrika Kusini imetangaza jambo jingine ambalo linazima kabisa majigambo ya wakosoaji wa Winnie.

Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri, Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma, akiwa na Waziri wa Habari, Nomvula Mokonyane, juzi aliviambia vyombo vya habari akiwa ndani ya Uwanja wa Orlando, shughuli za mazishi ya Winnie Madikizela-Mandela zitafanyika katika uwanja huo uliopo mjini Soweto na kushuhudiwa na mamia ya wabunge na wananchi wa nchi hiyo.

“Serikali yetu inathibitisha kuwa taratibu zote za kijeshi zitafanyika ili kutoa heshima ya mwisho kuaga mwili wa Winnie Mandela. Licha ya huzuni tuliyonayo, tunalazimika kukubali kuwa hayupo nasi tena duniani,” alisema Dlamini-Zuma.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles