Na Clara matimo, Mwanza
Katika kuitikia wito wa Serikali wa kufanya biashara kwa kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani badala ya madini ghafi, Chama cha Wanawake wachimbaji Wadogo wa Madini na Waongeza thamani madini (WIMO) kinatarajia kuanza kutengeneza na kuuza nguo, viatu na mikanda iliyonakshiwa kwa madini na Vito vinavyopatikana nchini.
Hayo yamebainishwa jijini Mwanza leo Mei 10, 2023 na Mwenyekiti wa WIMO Taifa, Mery James alipozungumza na MTANZANA DIGITAL katika Viwanja vya Rock City Mall ambako wiki ya maonesho ya madini, kongamano la Wachimbaji wa madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) vinafanyika.
Mery amesema wameamua kuja na ubunifu huo ili kuwa tofauti na wafanyabiashara wengine wanaoongeza thamani madini pia kupata faida zaidi katika shughuli zao za uchimbaji, kutangaza vivutio vya madini mbalimbali yaliyopo nchini na kuinua pato lao binafsi na taifa kwa ujumla.
“Malengo ya WIMA ni kuwasaidia wanawake wachimbaji wadogo wa madini nchi nzima tunataka mwanamke atoke katika kipato cha chini na utegemezi afike kipato cha kati kitakachomuwzesha kumudu kujikimu mahitaji yake yote muhimu.tunaamini mwanamke asipokuwa tegemezi hata ukatili wa kijinsia unapungua ndani ya ndoa na jamii.
“Tumeshanunua mashine yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu kwa ajili ya kudizaini na kunakshi nguo na mavazi ya jinsia zote ikiwemo mashati, magauni, viatu na mikanda tunapenda tuwe tofauti na wachimbaji au wafanyabiashara wengine katika sekta ya madini  maana biashara ni ubunifu, bidhaa tutakazotengeneza tutaziuza ndani na nje ya nchi.
“Lakini kwa kuwa sisi ni akina mama tunatarajia pia kuwafikia vijana ili kuwapa ajira nao waweze kujikwamua kiuchumi kupitia ubunifi wetu huo hasa kule Mkoani Tanga tutashirikisha sana kundi hilo maana fursa ni nyingi tunamiradi  mingi ya kuongeza thamani madini tunayoyachimba,” amesema Mary.
Amesema ingawa wana ndoto kubwa za kujiinua kiuchumi kupitia fursa ya aina mbalimbali za madini yaliyopo nchini lakini changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa mitaji kwani wanafanya shughuli zao katika mazingira magumu na kushindwa kuchimba kwa tija.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya WIMO, Jenipha Lulahobotse ameiomba Serikali itilie mkazo taasisi za fedha ziweze kuangalia namna ya kushirikiana na wachimbaji wadogo hasa wanawake ambao kwa asilimia kubwa huwa ni waaminifu  ikiwemo kuwakopesha wachimbaji kwani uchimbaji wanaoufanya sasa ni tofauti na wazamani ambapo walikuwa wakichimba kwa kubahatisha.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuweka  mazingira bora na rafiki kwa wachimbaji wadogo, ikiwemo kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili na kutatua kwa asilimia kubwa walizonazo, jana Mei 9, 2023 tumeshuhudia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizitolea maelekezo baadhi ya changamoto hizo namna jinsi ya kuzitatua baada ya Rais wa FEMATA, John Bina kuzitaja kiwemo tozo na ushuru zinazopangwa kupitia sheria ndogo ndogo za halmashauri bila kuwashirikisha wachimbaji alipofungua kongamano la wachimbaji wa madini.
“Hivyo naendelea kuiomba  serikali kutilia mkazo taasisi za fedha kuwakopesha wachimbaji maana kipato kikubwa kiko kwenye uchimbaji, ni kweli uchimbaji wa zamani ulikuwa wa kubahatisha lakini uchimbaji wa sasa ni wa  uhakika kwa sababu kabla ya kuanza shughuli ya uchimbaji mchimbaji anatumia vifaa vya kisasa kupima ili kuwa na uhakika kwamba eneo analochimba lina madini,” amesema Bina.