33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wilaya ya Ukerewe yajipanga zoezi la Sensa kuwafikia wavuvi

Na Clara Matimo, Ukerewe

Ingawa Wilaya ya Ukerewe iliyopo mkoani Mwanza inaundwa na Visiwa 38, kati ya hivyo 15 ni makazi ya watu ya kudumu, 23 ni makazi ya muda ambayo wavuvi huenda kufanya shughuli za uvuvi kisha kuondoka imetajwa kwamba si kikwazo katika kutekeleza zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 23, 2022.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Kanali Denis Mwila(kulia) akifurahia jambo kwenye bonanza la uhamasishaji sensa ya watu na makazi lililoandaliwa na halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe na kufanyika katika uwanja wa Getrude Mongella,  kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Emmanuel Sherembi.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 21, 2022 na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Denis Mwila wakati akizungumza na wananchi waliofika uwanja wa Getrude Mongella uliopo Nansio wilayani humo kwenye Bonanza la Uhamasishaji Sensa ya Watu na Makazi lililoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ambapo wananchi walishuhudia michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete na ngoma za asili.

Amesema wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha zoezi la sensa linafanikiwa ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo wameweka utaratibu mzuri na wavuvi hao pamoja na kuwahamasisha ambapo wamekubali kushiriki zoezi la sensa kikamilifu.

“Ninachotaka kuwaambia jiografia ya Ukerewe wala siyo kikwazo chochote cha watu kuhesabiwa kila mtu atakaye lala ndani ya mipaka ya wilaya hii atahesabiwa siku hiyo ya sensa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100.

“Katika visiwa vyote na mialo yote tumekwishaongea na wavuvi pamoja na viongozi wao wa kambi tumekubaliana siku ya sensa wataenda kuvua lakini alfajili watarudi kwa ajili ya kuhesabiwa na maeneo yote ya mialo yatakuwa ya kwanza kufikiwa saa 12 asubuhi makarani wa sensa watapita kwa ajili ya kuwahesabu wavuvi hao kabla ya kwenda kwenye kaya za wananchi,” amesema Kanali Mwila.

Wachezaji na mashabiki wa timu ya mpira wa pete ya Bukongo iliyopo wilayani Ukerewe wakiwa wanashangilia baada ya kuibuka washidni kwa kuichapa timu ya Kagera magoli 11 -9 na kupata zawadi ya mbuzi kutoka halmashauri ya wilaya hiyo ambayo walikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Kanali Mwila.

Kanali Mwila ambaye pia ni Mwenyekiti wa sensa wilayani humo amewasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa kwani zoezi hilo ni muhimu  ambapo aliwafafanulia kwamba linalenga kuchakata, kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi, kijamii na kimazingira ambazo zitaisaidia serikali kutengeneza sera kwa ajili ya maendeleo pia jinsi ya kupigana na maadui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi.

“Kutokana na sensa tutajua jinsi gani ya kuwawezesha wananchi kupata elimu kwa kujenga madarasa pamoja na vitu vyote vinavyohusiana na elimu, kupingana na umasikini takwimu hizo zitaisaidia serikali  kupanga jinsi gani wananachi wanaweze kuzalisha mali kwa kutumia rasilimali tulizonazo.

“Kwa  kupambana na maradhi  takwimu hizo zitaisaidia serikali kujua  namna gani tunaweza kupata madawa, kujenga zahanati, vituo vya afya na kutoa huduma zote za kiafya kwa wananchi,”ameeleza Kanali Mwila.

Mratibu wa Sensa Wilaya ya Ukerewe, Joachim Tungilo amesema ikiwa imabaki siku moja zoezi la sensa kufanyika hawana mashaka maana wanaamini litafanikiwa kwani viongozi wa vijiji, vitongoji na kata wameisha wahamasisha wavuvi wote ili washiriki zoezi hilo muhimu serikali iweze kupata takwimu yao kamili kwa ajili ya kuwaboreshea shughuli zao za uvuvi.

“Hata wananchi wote watakao lala katika nyumba za kulala wageni nao watafikiwa kwani tumeishapeleka fomu kwenye maeneo hayo lengo ni kuhakikisha hakuna mtu ambaye hatahesabiwa  ninachowaasa tu wananchi watoe taarifa zao sahihi ambazo wataulizwa na makarani wa sensa,” amesema Tungilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Sherembi amewasihi wakazi wa wilaya hiyo wajitokeze kuhesabiwa kwa maendeleo ya taifa.

Katika bonanza hilo timu ya mpira wa miguu ya Uvuvi Fc imeibuka kidedea kwa kuifunga Watumishi FC bao 1- 0 huku mpira wa ] pete timu ya Bukongo ikiichapa kagera magoli 11 -9 ambapo washindi walipewa zawadi ya mbuzi kwa kila timu.

Timu ya watumishi Fc imepewa zawadi ya fedha kiasi cha Sh 40,000  kwa kuibuka mshindi wa pili, Kagera Fc imepata Sh 30,000 kwa kushika nafasi ya tatu, Nansio Academy imeambulia Sh 15, 000 kwa kushiriki bonanza hilo kwa upande wa mpira wa pete timu ya kagera imeondoka na Sh 15, 000 .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles