24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wiki tatu kabla ya uchaguzi, kashfa zatumika kama mtaji

donald-and-hillary-2KAMPENI za kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu ya White House zinaendelea kupamba moto nchini Marekani huku kila mgombea akijitahidi kujinadi kwa wapiga kura kwa kumkosoa mpinzani wake.

Zikiwa zimesalia siku 20 kabla ya wapiga kura kumchagua mrithi wa Rais Barack Obama, kampeni za kipindi hiki cha lala salama zimekuwa za kufa na kupona zikijikita zaidi kushambuliana hasa upande wa mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump.

Huku wakitarajia kukabiliana katika mdahalo wao wa tatu na wa mwisho leo usiku, matokeo ya kura za maoni yanaonesha mpinzani wake kutoka chama cha Democratic, Hillary Clinton anaongoza kwa tofauti kuanzia asilimia nne hadi kuwa na tarakimu mbili.

Trump mara kwa mara anavishutumu vyombo vya habari kwa kumhujumu na kumpendelea mpinzani wake, sasa amerudia madai kuwa uchaguzi huo hautakuwa halali kwa vile chama cha Democratic kimepanga kuiba kura vituoni.

Hata hivyo, wakosoaji wake wakiwamo kutoka chama chake wameiponda kauli hiyo ya madai ya uwepo wa wizi wa kura wakisema ni ya mfa maji.

Tangu kuvuja kwa kanda ya video, ambamo Trump anasikika akijigamba namna anavyowachezea wanawake wakiwamo wake za watu kwamba wanajipeleka wenyewe kwake kutokana na umaarufu, kambi ya Clinton imeongeza mashambulizi zaidi kupitia tuhuma hizo.

Licha ya kwamba Trump alikana tuhuma hizo, akisema kilichosikika katika kanda hiyo ni mazungumzo ya mzaha chumbani yasiyoendana na tabia na haiba yake, wanawake sita wamejitokeza kumpinga.

Wanawake hao waliojitokeza kwa nyakati tofauti tangu Trump akane wakati wa mdahalo wa pili uliofanyika Jumatatu iliyopita, wamesimulia namna walivyokuwa wakidhalilishwa na bilionea huyo huko nyuma kinyume na makano yake.

Clinton, malkia wa vigogo wa siasa za Washington, anahesabiwa kwamba mlaghai na mwongo anadaiwa kuwa kipenzi cha tabaka fulani teule la matajiri analolenga kulilipa fadhila kwa misaada yao kwa taasisi ya familia-Clinton Foundation.

Kwamba tabaka hilo liko nyuma ya vyombo vya habari kufumbia madhambi ya Clinton yanayozidi kufichuliwa na mtandao wa Wikileak kwani kumlenga zaidi Trump.

Lakini pia Trump ametumia miaka mingi akijitapa kila aina ya majigambo kuanzia utajiri, unadhifu wake hadi kwa kuwadhalilisha wanawake.

Lakini sasa amechukizwa na tuhuma hizo za udhalilishaji kingono ambazo amezikana kiasi cha kutoa vitisho vya kumfunga Clinton na kuwashughulikia wapinzani wake wengine.

Miongoni mwa alioapa kuwashughulikia akiingia madarakani ni Spika wa Bunge la Marekani kutoka chama chake, Paul Ryan, ambaye hivi karibuni alisema hatamuunga mkono Trump badala yake kusaidia wabunge na wawakilishi wao, akipinga kauli za ovyo za bilionea huyo kuhusu wanawake.

Lakini pia wote Clinton na Trump wanafahamika katika katika Sayansi ya Siasa kinajulikana kama ‘statists’ yaani wenye imani kwamba serikali inapaswa kudhibiti sera za kiuchumi au kijamii au zote kwa pamoja huku wakiamini katika matumizi ya madaraka kubomoa wenzao.

Clinton atachagua waliberali kuingia katika mahakama ya juu kwa ajili ya kutimiza matakwa yake huku Trump akiwa ameshaahidi kuchagua wahafidhina kuingia mahakamani.

Yote hayo ni kwa sasbabu mfumo nchini humo kwa sasa unanuka ufisadi, maadili kuporomoka kwa miaka kadhaa sasa bila kushughulikiwa huku wananchi wakilia na uongo wa wanasiasa nchini humo, ambao Trump na Clinton ni miongoni mwao kitu kinachowafanya wawe wagombea urais wanaochukiwa zaidi katika historia ya kisasa ya Marekani.

Kampeni ya Clinton imejikita katika kutumia historia ya Trump ya tuhuma za kudhalilisha wanawake kumharibia kwa wapiga kura wanawake.

Na hiyo ni muhimu sana kwa Clinton kwa sababu inavifanya vyombo vya habari viangazie katika suala hilo linalouza zaidi na kupuuza barua pepe zinazovujishwa na mtandao wa Wikileak, ambazo zinaweza kumbomolea kampeni yake.

Wakati Trump anakana tuhuma za udhalilishaji wanawake, analipia majigambo yake kwa gharama kubwa, licha ya kujaribu kuzipuuza akijikita kuvusha madai ya kila aina kuhusu Clinton ikiwamo ubovu wa afya yake akitaka kabla ya mdahalo wa leo wapimwe utimamu wa kimwili na kuangalia iwapo wanatumia dawa za kuongeza nguvu kama zile za michezoni zilizopigwa marufuku.

Clinton kwa upande wake, akidaiwa kuwa mwezeshaji na mtetezi wa uhuni wa mumewe, Rais wa 42 wa Marekani Bill Clinton, kwa sasa anachekelea ushindi kwa jinsi alivyojipanga akielekea kupata kile anachotaka;madaraka.

Wanawake wamemiminika kusimulia, simulizi ambazo baadhi ni za miaka 40 iliyopita, zilizokanwa vikali na Trump, lakini zilizotimiza malengo katika televisheni na kwa Clinton.

Clinton anajua nini cha kufanya kushinda kupitia mbinu na mikakati, akitumia hisia zaidi pamoja na tuhuma hizo za ngono zinazomwelekea Trump kupoteza malengo kumhusu na kuhakikisha kampeni haiingiliwi na kashfa nyingine katika wiki tatu hizi zilizobakia kabla ya upigaji kura Novemba 8.

Wakati wa mdahalo wa pili wa urais, Trump alikosolewa kwa kumfuata fuata kwa nyuma Clinton wakati akizungumza, kitu kilichodakwa na Clinton aliyewaambia wafuasi wake hivi majuzi kwamba alikuwa kana kwamba anaelekea kuvamiwa na mnyama.

Ni kwa sababu ya mbinu hizo za timu ya Clinton, kashfa ya barua pepe zilizovujishwa imepuuzwa.

Barua pepe hizo za karibuni pamoja na mambo mengine zinafichua ndoto ya Clinton ya kufungua mipaka ya Marekani kuwa huru zaidi kibiashara kupitia hotuba yake aliyolipwa kiasi kisichopungua dola 250,000 sawa na Sh million 500 kwa wawekezaji wa kibenki wa Brazil.

Kitendo hicho Trump anakiita mpango wa siri wa Clinton kuiuza Marekani kupitia kufungua milango wazi pasipoangalia maslahi ya Marekani.

Pia zinafichua uwezekano wa uwepo wa mgongano baina ya wizara mbili za ulinzi na mambo ya nje ili kumlinda Clinton dhidi ya kushitakiwa katika kashfa ya matumizi ya barua pepe binafsi pamoja na majadiliano ya kupata fedha nyingi kutoka kwa matajiri wa Saudi Arabia ilihali akijua ni wafadhili wa kundi la kigaidi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles