28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wiki nzito mjadala wa bajeti 2019/20

Na WAANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

WAKATI kesho wabunge wakitarajiwa kuanza kujadili Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2019/20, dalili zinaonyesha hoja nyingine nyingi zitaibuliwa bungeni. 

Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili jana  kuhusu mapendekezo hayo ya Serikali ya bajeti ya Sh trilioni 33.1, walisema licha ya kufutwa kwa tozo nyingine  bado wanazo nyingine ambazo watazifikisha bungeni.

Maeneo kadhaa ambayo tayari wabunge wameazimia kuelekeza ni pamoja miradi ya maendeleo, kodi, wafanyabishara, mishahara na madeni ya watumishi, taulo za kike, mawakala wa forodha na mengine.  

Wakati wabunge wakitazamia kuja na mjadala mpana kuhusu mapendekezo hayo baadhi ya wasomi na wadau mbalimbali wa maendeleo wameichambua bajeti hiyo katika mtazamo wa sura mbili.

Bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni Ijumaa wiki hii na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango, ambapo alitangaza kufuta tozo 54.

Tozo hizo zilikuwa zikitozwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mkemia Mkuu wa Serikali na kwenye sekta mbalimbali.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na MTANZANIA Jumapili wamesema bado kuna mambo mengi ya kujadili kuhusiana na mapendekezo hayo.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Ruth Mollel alisema yeye kama mtaalam wa Rasilimali Watu bado anaona maeneo kadhaa manne yanahitaji mjadala katika mapendekezo hayo ya bajeti.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja watumishi kupandishiwa  mishahara, kilichokwaza wafanyabiashara hadi kufunga biashara zao na suala zima la kodi.

Kuhusu mishahara Ruth alisema ataibua mjadala wa haja ya kuwepo fedha za kutosha zitakazopelekwa kuongeza mishahara ya watumishi,  kupandishwa vyeo na kulipa madeni yao.

Aidha alisema atataka kujua mpango wa serikali kulipa madeni yake inayodaiwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha inakuwa endelevu na malipo yanafanyika kwa wakati. 

Kuhusu biashara, alisema licha ya uamuzi wa serikali kuanzisha utaratibu mpya wa kutofunga biashara hadi pale kwa kibali cha Kamishna wa TRA, pia kufungua dirisha maalumu la kusikiliza kero zao ikiwamo makadirio ya kodi lakini anaona mjadala unahitajika kujua chanzo cha biashara nyingi kufungwa.

“ Biashara nyingi zimefungwa, watafute chanzo, hii inaathiri watu wengi kama mfanyabiashara anategemewa na watu wanane angalia wanaoathirika ni wengi, kama kodi zimezidi zipuondolewe,” alisema Ruth ambaye alisema uamuzi wa kuondoa tozo ni jambo jema, lakini kuwezesha biashara mpya ni jambo jema zaidi.

Mbunge wa Jimbo la Monduli (CCM) Julius Kalanga mbali na kupongeza mapendekezo hayo aliyosema yamegusa kero nyingi za muda mrefu katika sekta ya mifugo kwa maana ya maziwa na nyama, alisema serikali pia inapaswa kupima mjadala mwingine wa kushusha tozo ya usafishaji ng’ombe nje ya nchi kutoka shilingi 30,000 hadi 15,000 .

Kuhusu vyanzo vipya vya ukusanyaji mapato katika bajeti ya sasa Kalanga alisema hajaona zaidi ya vingi kubaki vile vile vya zamani na hivyo kushauri iwekeze kwenye viwanda ili ipate kodi zaidi.

Pia anasema sekta ya kilimo nayo inahitaji mjadala kwa serikali kufanyia marekebisho na kuongeza bajeti kwa ajili ya utafiti wa mbegu.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza ambaye amekuwa  akisimamia hoja ya kufutwa kwa kodi kwenye taulo za kike amesema uamuzi wa kuondoa msamaha kwenye taulo hizo si sahihi na kwamba suala hilo analirudisha tena bungeni.

“Sio sahihi, tatizo kubwa ni usimamizi, waliokuwa wanapandisha bei ni wafanyabiashara wa rejareja, kwa mfano always wao walipunguza kabisa bei na wakaandika kwenye pakiti Sh 1,500 lakini wauzaji wa rejareja waka wanauza Sh 2,000 hadi 2,500.

“Mimi ninachokiona hapa suala ni usimamizi serikali imeshindwa kuweka usimamizi ilifanya hivyo hata kwenye mafuta ya taa baada ya kuibuka uchakachuaji licha ya bidhaa hiyo kutegemewa na umaskini wao badala ya kutafuta njia ya kusimamia bei iwezi kumnufaisha Mtanzania wa hali ya chini wakaongeza bei sawa na mafuta ya petroli Sh. 2300-2,400, badala ya kuweka usimamizi inaongeza kodi,” alisema Upendo.

Kuhusu kuleta nafuu kwa mwekezaji wa ndani anayeanzisha viwanda vitakavyozalisha bidhaa hiyo, Upendo alisema hilo punguzo la miaka miwili si la kudumu.

“Tufanye uamuzi wa kudumu, nitasema kuna haja ya kulirudisha hili suala upya kwa sababu wasichana wengi wanaathirika na hili.” 

Pamoja na kuanzisha kodi mpya ili kulinda uwekezaji wa ndani, umeme unaouzwa Zanzibar umefutiwa kodi ya VAT ya asilimia 18 huku watumiaji wa bara wakiendelea kulipa asilimia 18 ya VAT.

Bajeti hiyo pia imeshuhudia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikipigwa marufuku kufunga biashara kwa sababu ya madeni na kwamba uamuzi huo sasa utafanywa kwa kibali maalumu cha kamishna na si vinginevyo.

Tofauti na bajeti zilizopita ambazo mara nyingi zilikuwa zikiongeza ushuru kwenye bia na sigara, hii haujaongezwa wala kupunguzwa.

Tozo zilizoongezwa katika bajeti ya sasa ni pamoja na ile ya leseni ya udereva ambayo  imepandishwa kutoka Sh 40,000 hadi  70,000, ada ya usajili wa magari 10,000-50,000, Bajaji 10,000-30,000, Pikipiki 10,000-20,000.

Kufutwa msamaha wa kodi kwenye taulo za kike,pia nywele za bandia  kutoka nje kuingia kwa mara ya kwanza kwenye tozo ya asilimia 25 ni baadhi ya hoja ambazo zinategemewa kusikika ndani ya Bunge.

Aidha uamuzi wa serikali kuruhusu mtu mmoja mmoja aweze kutoa mizigo yake bandarini bila kutumia  Wakala wa Forodha nao unaweza kuamsha mjadala bungeni.

Tayari Chama Cha Mawakala wa Forodha (TAFA) kimesema kinajiandaa kwenda Dodoma kwa ajili ya kupeleka hoja zao kuishauri serikali kuachana na uamuzi huo.

TAFA kinasema kuwa uamuzi huo unaoziweka hatarini ajira zaidi ya 10,000.

Jana chama hicho kilijifungia kujadili uamuzi huo na kuja na mapendekezo ya namna ya kuishauri serikali.

Gazeti hili pia linazo taarifa kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nacho jana  kilifanya mkutano wake wa ndani kujadili mapendekezo hayo ya bajeti na hoja watakazopeleka bungeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles