Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Afya Duaniani (WHO), limekubaliana na hoja za Rais Dk. John Magufuli kuhusu mapambano dhidi ya corona ikiwamo suala la ugonjwa huo kuishi kama ilivyo kwa maradhi mengine kama Virusi vya Ukimwi.
Mei 3, mwaka huu Rais Magufuli, wakati akihutubia taifa, alisema kuwa uzoefu unaonesha ni kawaida kuwa kila gonjwa jipya linapotokea watu hupata wasiwasi kama ilivyotokea kwa ugonjwa wa Ukimwi lakini hata watu waliobainika kuambukizwa Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza katika moja ya vikao vyake hivi karibuni, Mkurugenzi wa dharura wa WHO, Dk. Mike Ryan, alionya dhidi ya kujaribu kubashiri ni lini virusi vya corona vitatoweka.
Aliongeza kuwa kama chanjo itapatikana, kudhibiti virusi kutahitaji “juhudi kubwa” katika kuvitokomeza.
“Ni muhimu kufahamu hili, virusi vinaweza kuwa janga jingine katika jamii zetu na virusi hivi huenda visiishe,” alisema Dk. Ryan alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Geneva.
“Virusi vya HIV havijaisha – lakini tumevizoea,”
Dk. Ryan alisema pia kwamba haamini “mtu yeyote anaweza kubashiri ni lini ugonjwa huu utatoweka”.
Kwa sasa kuna chanjo zaidi ya 100 zinazofanyiwa utafiti- lakini Dk. Ryan alisema kuna magonjwa mengine, kama vile tetekuwanga, ambayo bado hayajatokomezwa licha ya kuwa kuna chanjo yake.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, alisisistiza kuwa bado inawezekana kudhibiti virusi vya corona, kwa juhudi.
“Suluhu liko mikononi mwetu, na ni shughuli ya kila mtu, na sote tunapaswa kuchangia kuzuia janga hili,” alisema.
Mtaalamu wa WHO wa majanga, Maria van Kerkhove pia ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa jamii inapaswa kuweka akilini kwamba itachukua muda kuondokana na janga hilo.
Kauli zao zinakuja huku nchi mbalimbali zikianza kulegeza hatua za kukaa nyumbani na viongozi wanaangalia uwezekano wa lini na ni vipi wanaweza kufungua shughuli za kiuchumi katika nchi zao.
Dk. Tedros alionya kuwa hakuna hakikisho juu ya njia za kulegeza hatua za kukaa nyumbani bila kusababisha wimbi jingine la maambukizi.
“Nchi nyingi zingependa kuacha hatua tofauti za kukabiliana na virusi.
“Lakini pendekezo letu ni kwamba kukapa chanjo kunahitajika bado katika kila nchi kwa kiwango kiwezekanacho,” alisema Dk. Tedros.
Aidha, Dk. aliongeza kuwa kuna fikra za ajabu zinazoendelea kwamba sheria ya kukaa nyumbani inasaidia kabisa na kwamba kuondolewa kwake kutakuwa vizuri na kwamba yote yanaweza kusababisha hatari.
Takribani watu 313,771 kote duniani wameripotiwa kufa kutokana na virusi vya corona na zaidi ya visa milioni 4.7 vimerekodiwa duniani kote.
Upuliziaji dawa
Mwishoni mwa wiki Shirika la Afya duniani (WHO) lilionya kuwa kutumia dawa ya kuua viuatilifu barabarani, kama inavyofanywa katika baadhi ya nchi ikiwamo Tanzania, hakuondoi virusi hivyo vipya na badala yake kunahatarisha Afya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na WHO ilisema kuwa kupulizia dawa mitaani na usoni hakuwezi kuwa na tija katika kukabiliana virusi vya corona.
“Kupulizia dawa usoni, mitaani, sokoni siyo jambo linalofaa kwa kuwa haiui virusi vya COVID-19 au vimelea vingine kwa sababu hiyo inaondoa viuatilifu tu vilivyojificha kwenye uchafu. Hivyo licha ya kukosekana kwa tiba lakini bado dawa ya kunyunyizia kemikali haiwezi kuua virusi vya corona,” ilisema taarifa hiyo ya WHO.
Aidha, WHO kupitia taarifa hiyo ilisema kuwa mitaani na maeneo mengine kama sokoni kusichukuliwe kama sehemu iliko “hifadhi ya maambukizi” ya COVID-19, na kuongeza kwamba dawa viini, hata nje, inaweza kuwa “hatari kwa afya ya binadamu,” alisema.
Shirika hilo lilionya kuwa njia hiyo haifai katika hali yoyote ile.
Mei 3, mwaka huu Rais Magufuli alieleza kuwa uzoefu unaonesha ni kawaida kuwa kila gonjwa jipya linapotokea watu hupata wasiwasi kama ilivyotokea kwa ugonjwa wa Ukimwi lakini hata watu wanaobainika kuambukizwa Virusi vya Ukimwi wanakwenda kuposa na kuoa.
Alisema wakati wa ugonjwa wa surua ilikuwa marufuku hata kwenda kutembelea eneo hilo na imekuwa hivyo hivyo kwa magonjwa kama ukoma na Kifua Kikuu (TB), ebola, zika, hofu zimekuwa zikijengeka lakini matatizo hayo hatimaye yalipatiwa ufumbuzi.
Alisema corona kweli ipo lakini isiyumbishe Watanzania katika msimamo na mwelekeo, wasitishwe na aliendelea kutoa wito hasa kwa vijana ambao muda mwingi wanapost watu wakisema wamekufa kwa corona.
Licha ya hali hiyo alipiga marufuku suala la upuliziaji dawa kwa ajili ya kuua virusi vya corona huku akiagiza walioamuru suala hilo lifanyike wachunguzwe kwani huenda kulikuwa na ulaji wao.