SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limesema kuna maambukizi mapya milioni moja ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya zinaa kila siku.
Hiyo inamaanisha kuwa zaidi ya maambukizi mapya milioni 376 hutokea kila mwaka yakiwemo magonjwa ya kisonono, kaswende Chlamydia na trichomoniasis.
WHO imesema ukosefu wa mafanikio ya kuzuwia kuenea kwa magonjwa ya zinaa ni moja ya sababu za kuenea kwa kasi kiwango hicho cha maambukizi hivyo hatua za dharura kukabiliana hali hiyo zinahitajika.
Wataalamu zaidi wanahofu juu ya kuongezeka kwa visa magonjwa ya zinaa kuwa sugu kiasi cha kutotibiwa na dawa zilizopo kwa sasa.
Shirika la WHO mara kwa mara hutathmini athari za magonjwa manne ya zinaa ambayo yamekuwa yakiripotiwa zaidi maeneo mengi duniani.
Shirika hilo liliangalia utafiti uliochapishwa na kukusanya ripoti kutoka kwa wafanyakazi wake katika nchi mbalimbali zikilinganishwa na tathmini ya mwaka 2012 .
Shirika hilo linasema mtu mmoja kati ya 25 duniani ana walau aina moja ya maradhi ya zinaa, huku baadhi wakiwa na maambukizi ya magonjwa zaidi moja kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mwaka 2016 watu wenye miaka 15 hadi 49, milioni milioni 156 walikuwa na trichomoniasis, milioni 127 walikuwa na Chlamydia, milioni 87 walikuwa ni wagonjwa wapya wa Kisonono na watu milioni 6.3 walikuwa ni wagonjwa wapya wa kaswende.
Trichomoniasis husabishwa na maambukizi ya vimelea wakati wa ngono. Chlamydia, kaswende na kisonono ni maambukizi ya bakteria.
Dalili za magonjywa ya zinaa ni pamoja na kutokwa na majimaji yasiyo ya kawaida kwenye uke au uume, maumivu wakati wa kwenda haja ndogo na kuvuja damu kabla ya muda wa hedhi.
Madhara makubwa mtu anayoweza kuyapata kutokana na Trichomoniasis ni pamoja na kupata maradhi ya majeraha ya kiunoni na kukosa uwezo wa kupata ujauzito kwa wanawake ama kutungisha mimba huku Chlamydia, kisonono na kaswende zikitajwa kuwa ni magonjwa yanayoweza kusababisha maradhi ya moyo.
Kama mwanamke ataambukizwa ugonjwa wa zinaa iwapo ni mjamzito anaweza kujifungua mtoto mwenye ukosefu wa baadhi ya viungo vya mwili au kujifungua mtoto njiti, mwenye uzito wa chini na huenda akawa na matatizo mengine ya kiafya kama kichomi, upofu na kuzaliwa na kasoro katika viungo vyake vya uzazi.
Daktari Peter Salama wa WHO, alisema “tunashuhudia ukosefu wa mafanikio ya kuzuwia usambazaji wa magonjwa ya zinaa kote duniani. Huu ni wito wa kufayika kwa juhudi za pamoja kuhakikisha kila mmoja popote alipo anaweza kupata huduma anazohitaji kuzuwia na kutibu magonjwa haya.”
WHO inasema kufanya ngono salama hususani kwa kutumia mipira ya kinga na upatikanaji mzuri wa vipimo vya maradhi vyote ni muhimu.
Kwa upande wa matibabu, magonjwa ya zinaa yatokanayo na na bakteria yanaweza kutibiwa kwa dawa zilizopo.
Lakini tiba ya kaswende imekuwa ni ngumu zaidi kwasababu ya ukosefu wa aina ya kipekee ya dawa ya penicillin inayohitajika na kumekuwa na ongezeko la kile kinachoitwa “kisonono sugu ”