23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

WHI yatakiwa kuchukua Mfuko wa Mikopo kwa Watumishi wa Umma

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirika la Watumishi Housing Investment (WHI) limehimizwa kufuatilia na kuchukua usimamizi wa mfuko wa mikopo kwa watumishi wa umma, ambao kwa sasa upo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ili kuimarisha huduma za makazi kwa watumishi.

Rai hiyo imetolewa leo, Agosti 19, 2024, na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, wakati wa ziara yake katika Shirika hilo na alipotembelea nyumba zao zilizopo Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa WHI, Fredy Msemwa(aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa ziara hiyo.

“Mfuko huo ni muhimu sana kwa sababu watumishi wanakutana na changamoto nyingi. Kupitia Watumishi Housing Investment, tunaweza kupata suluhu ya matatizo ya watumishi, hasa katika suala la makazi. Tukifanikiwa kuwa na mifuko imara, tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kutatua matatizo ya watumishi,” alisema Sangu.

Aidha, Naibu Waziri Sangu alisisitiza umuhimu wa WHI kuweka utaratibu mzuri wa makusanyo ya fedha kwa watumishi wanaokopeshwa nyumba, akitahadharisha juu ya baadhi ya watumishi ambao hawana uaminifu katika ulipaji wa mikopo.

“Suala hili lipo ndani ya Serikali, kila mtumishi ambaye amekopeshwa nyumba ahakikishe analipa fedha hizo ili ziweze kutumika katika miradi mingine ya ujenzi wa nyumba kwa watumishi,” aliongeza.

Pia, Sangu aliwahimiza WHI kuendelea kusimamia mfuko wa uwekezaji wa FAIDA FUND kwa njia za kisayansi na kitaalamu, ili kuhakikisha wawekezaji wanapata imani na kuvutiwa kuwekeza zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WHI, Fredy Msemwa, alisema kuwa moja ya malengo ya kuanzishwa kwa Shirika hilo lilikuwa ni kuhamishia mfuko wa mikopo kwa watumishi wa umma chini ya WHI. Hata hivyo, alikiri kuwa juhudi hizo zimekwama kutokana na masuala ya kisera na kiuendeshaji.

“Sehemu kubwa ya fedha za mfuko huo tayari zimekopeshwa, hivyo utaratibu wa kuuhamishia hapa bado unafanyiwa kazi. Tunaomba muda zaidi ili kuendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi kutafuta njia ya haraka zaidi ya kufanikisha suala hili,” alisema Msemwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles