32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wezi wa nyaya za umeme Bukoba wasakwa

Na Nyemo Mlecela, Kagera

SERIKALI ya Mkoa wa Kagera imeanza kuwasaka watu wanaohujumu miundombinu ya umeme wilayani Bukoba inayosababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara na hivyo kulisababishia hasara Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo.

Hatua hiyo imefikiwa leo Jumanne Julai 20, 2021 baada ya Tanesco kuwasilisha changamoto ya uharibifu wa miundombinu kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ili aweze kuwaongezea nguvu katika msako wa kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma.

Kufuatia vitendo hivyo kukithiri, Machali ameliagiza Jeshi la Polisi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tanesco katika zoezi la kuwasaka watu wote waliohusika na vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme.

“Jeshi la polisi na Tanesco mnatakiwa kuanza msako huo kwa kuwakama waliochoma nguzo, mkikuta nguzo imeungua katika shamba la mtu muanze na mmiliki wa shamba hilo, hivyo watendaji wa vijiji na kata fanyeni uchunguzi kabla ya kuja kuulizwa na mkuu wa wilaya, polisi au Tanesco na kutoa taarifa mapema na msipofanya hivyo tutawachukulia hatua kwa kufanya uzembe wa kutowatafuta wale ambao wamekuwa wakifanya hujuma hizo,” amesema Machali.

Pia Machali amewaagiza watendaji wa mitaa, vijiji, kata na maafisa tarafa kuhakikisha wanachukua jukumu la ulinzi wa miundombinu hiyo ili kuhakikisha inakuwa salama katika maeneo yao. Kwa mujibu wa sheria ya mamlaka ya serikali ya mitaa ya mwaka 1982 kama ilivyofanyiwa marejeo, wao ni walinzi wa amani katika maeneo yao, kwa hiyo wao wanao wajibu wa kuhakikisha kuna ulinzi na amani kwa wananchi na mali zao.

Hivyo, hujuma hizi zinapotokea nataka nikiwauliza watendaji waniambie wamechukua hatua gani kufanya uchunguzi, wamewapata au hawajawapata watu waliofanya vitendo hivyo, mfano vitendo vya uchomaji moto nguzo za umeme ambavyo vinatokana na wananchi kusafisha mashamba yao kwa kuchoma moto vichaka jambo ambalo linasababisha nguo za Tanesco ambazo ni za miti kuungua.

Aidha, ameagiza kuwa kila mwananchi anatakiwa kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo ili kusaidia kupunguza katizo la umeme la mara kwa mara kwa kuwa nishati hiyo ni muhimu kwa wananchi wote wa wilaya hiyo.

Machali amezitaja baadhi ya hujuma ya miundombinu iliyofanywa kwa shirika la Tanesco kuwa ni pamoja wizi wa waya wa umeme wenye urefu wa mita 70, tukio lililofanywa Februari 2, mwaka huu katika maeneo ya Nyanga, Kyakailabwa Manispaa ya Bukoba wakati Aprili 19, mwaka huu huko eneo la Gera Kashasha Kikukwe pia kulifanyika wizi wa waya wa umeme wenye urefu wa mita 60 na kusababisha katizo la umeme katika maeneo hayo.

“Tukio lingine la wizi lilifanyika huko Izimbya A hospitali Juni 16, mwaka huu ambapo wezi hao waliiba nyaya za kopa kwenye transifoma na kusababisha hospitali hiyo kukosa umeme na kuathiri utoaji wa huduma kwa wagonjwa hasa waliokuwa wanapatiwa huduma kwa kutumia mashine.

“Na Juni 25, mwaka huu kumetokea wizi wa waya wa umeme wenye urefu wa mita 150 maeneo ya Kilima, Kabanga Katoma wakati Julai 8, mwaka huu kulitokea kitendo cha uchomaji moto nguzo mbili za umeme huko Mugana Katale, Julai 12 mwaka huu huko Kemondo Kyetema kulitokea vitendo vya uchomaji moto wa nguzo za umeme, Julai 14, mwaka huu kulitokea kitendo cha kukatwa kwa waya kwenye laini kuu ya gridi ya umeme unaotoka nchini Uganda jambo ambalo litasababisha tukose umeme kwa siku zisizopungua mbili,” amebainisha Machali.

Ameongeza kuwa vitendo hivyo vya kuhujumu miundombinu ya umeme vinaweza vikasababisha vifo kwa watu ambao wanahitaji huduma ya kitabibu kwa kutumia mashine zinazotumia umeme lakini pia kuisababishia hasara jamii ambayo inategemea nishati hiyo kufanya biashara zao na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.

“Mfano jambo la kukata waya kwenye laini kuu ya gridi ya umeme kutoka Uganda na transifoma ni hatari kwani linaweza kusababisha watu wakapoteza maisha, hivyo kila mwananchi anatakiwa kuwa mlinzi wa miundombinu hii ili kuhakikisha Tanesco haikumbwi na changamoto ya kukosekana kwa umeme kutokana na kuingia hasara katika uwekezaji wa kununua nguzo, nyaya na vifaa vingine vinavyosaidia kusambaza umeme kwa wananchi wa mijini na vijijini,” amesema Machali.

Naye Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja wa Tanesco Kagera, Samweli Mandali amesema katika kumbukumbu za shirika hilo, kitendo cha kuibiwa kwa nyaya katika laini kuu ya gridi ya umeme kutoka nchini Uganda ni cha kwanza kujitokeza.

“Hujuma kama hii kwenye miundombinu kunachangia kukatika kwa umeme na kumbukumbu zinaonyesha katika kipindi cha kiangazi, watu wanaandaa mashamba kwa kuchoma moto jambo ambalo linasababisha nguzo za umeme kuungua, matukio yanayojitokeza mwaka hadi mwaka na  vitendo hivyo vimekuwa vikijitokeza mara nyingi katika wilaya za Bukoba, Karagwe na Kyerwa,” amesema Mandali.

Ameongeza kwa kuwataka wananchi waliounganishwa kwenye mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao ulizinduliwa na Naibu Waziri wa Nishati, Adv. Steven Byabato mwezi uliopita wazingatie taratibu zilizowekwa na serikali pamoja na shirika hasa viwango vya gharama za kuunganishiwa umeme.

“Niwatake wananchi kuacha tabia ya kutumia wakandarasi vishoka kwa kuwa wanafanya kazi chini ya viwango, kuepuka kupoteza fedha nyingi kwa sababu vishoka hao wanatoza gharama kubwa lakini pia kuwatoza fedha baadhi ya vifaa ambavyo vinatolewa bure na Tanesco.

“Serikali ilishatoa maelekezo kuwa gharama za kuunganishiwa umeme ni Sh 27,000 na wananchi wanatakiwa kufuata utaratibu huo, pia wananchi wanatakiwa kutumia wakandarasi wanaotambulika na siyo kutumia vishoka kwani wanaweza kuwasababishia madhara ya kuunguliwa na nyumba zao,” amesema Mandali.

Upande wake Mkazi wa Bilele Manispaa ya Bukoba, Shaff Jumanne amesema kuwa umeme ni kiinua mgongo cha uchumi wa nchi kwa kuwa unategemewa zaidi na wafanyabiashara wadogo hadi wakubwa katika uzalishaji wao wa kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles