24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wewe siyo wa kwanza kuanzia sifuri!

Jessica-Valenti-Sad

Na ATHUMANI MOHAMED

MATAJIRI wengi hawapendi kueleza siri zao za mafanikio na namna walivyoibuka na mabilionea. Lakini habari nzuri kwako ni kwamba, asilimia kubwa ya matajiri wameanzia chini kabisa nikimaanisha sifuri.

Usigope umasikini wako, ni suala la muda na kujipanga. Ni kweli kuwa fedha ni kitu muhimu katika maisha yetu. Ukiweza kuwa na fedha za kutosha, ni wazi kuwa inaweza kuwa njia ya kukufanya uweze kuanzisha miradi mingi na hatimaye kutajirika.

Bahati mbaya, wengi hufikiri ukiwa huna fedha basi ni vigumu kupata fedha zaidi. Huwezi kuwa tajiri. Kuna msemo unasema: Maji hufuata mkondo. Wapo wanaokwenda mbele zaidi wakiufananisha msemo huu na fedha.

Kuwa mwenye fedha ndiye pekee anayeweza kuendelea kuwa na fedha nyingi zaidi wakati asiye nazo akibaki katika umasikini wa kutupwa! Si kweli.

Huko mbele nitakwenda kutoa mifano halisi ya watu ambao walizaliwa kwenye familia maskini, wakiwa hawana kitu kabisa lakini wakaanzia sifuri na sasa ni matajiri.

Swali ni je, ukiwa huna fedha kabisa unaweza kutajirika? Jibu ni ndiyo. Lakini katika mada hii tutaona japo kwa muhtasari namna ambavyo unaweza kutajirika baada ya kuweka malengo.

UMIZA KICHWA

Baadhi ya watu hawatumii ubongo wao sawasawa katika kujitafutia maendeleo. Ukiachana na maendeleo, kuna watu  hufanya mambo bila kufikiria. Ubongo ndiyo injini ya maisha ya binadamu.

Tuliza kichwa, fikiri. Hakuna jibu baya kwenye kufikiri kama utakuwa umeutuliza ubongo wakati wa zoezi hilo. Kumbuka huna kitu na unataka kufanikiwa kimaisha, lazima uwe na hasira na mafanikio.

Uwe na chuki na umaskini, ndipo fikra zako zinaweza kuwa zenye maana na matokeo mazuri zaidi. Fungua ubongo wako, fikiri kitu cha kufanya. Jiulize: “Hivi nifanye nini duniani ili niweze kubadili maisha yangu?”

Jibu utakalopata hapo litakupa mwanzo mzuri wa hatua inayofuata.

TAFUTA WAZO LA BIASHARA

Ukiacha ubongo wako ufikiri sawasawa sasa ni wazi kuwa utakuwa na utulivu wa kufikiri kuhusu wazo la kitu cha kufanya. Unaweza kufanya nini? Biashara, ajira, sanaa au nini? Kuna watu hawaelewi, si kila utajiri lazima utokane na biashara.

Wengi hufikiri kuwa lazima fedha iingie kwenye mzunguko ndipo uweze kupata fedha nyingine, si kweli. Unaweza kutumia kipaji chako ukatengeneza fedha nyingi.

Kikubwa ni kuangalia njia (wazo) ya mahali pa kutokea kama kianzio. Mfano, wapo wasanii kadhaa hapa nchini wamefanikiwa kupitia vipaji vyao.

Wapo waliowaajiri vijana wenzao na wengine kufungua biashara nyingine nyingi nje ya sanaa na zinafanya vizuri. Mfano mwanamuziki Diamond, licha ya kwamba yeye mwenye amefanikiwa kutokana na muziki ameweza kufungua lebo ya WCB ambayo ina wanamuziki wenzake wa Kitanzania.

Zingatia jambo moja kubwa nililoeleza katika kipengele hiki, tafuta wazo. Kitu gani kinaweza kukutoa?

FUKUZIA NDOTO YAKO

Anza kujaribu kufanya kile ulichowaza. Katika kipindi hiki usiwe mtu wa kukata tamaa mapema. Wanasema, mwanzo mgumu hivyo lazima ukubaliane na changamoto zote utakazokutana nazo wakati ukijaribu kupambana.

Jifunze kupitia kwa watu, tafuta maarifa kutoka kwa watu ambao tayari wameshafanikiwa kupitia kitu unachotaka kufanya. Angalia mawazo yao, yachukue, boresha kisha ufanye kwa juhudi zaidi.

Wiki ijayo tutaendelea na mada hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles